“Upo sehemu ulipo leo sababu mawazo yako yamekufikisha hapo ulipo. Kesho utakuwa pale mawazo yako yatakapo kufisha.”James Allen.
Ulimwengu wako wa nje unatawaliwa na ulimwengu wa ndani yaani mawazo
yako. Ubora wa ufahamu wako au fikira zako ndiyo unatangaza hatima ya maisha
yako ya kesho. Kama mawazo ndiyo yanaongoza maisha yako basi kuwa na ufahamu
wenye nguvu ni muhimu sana. Kuwa na ufahamu legevu ni hatari sana kuliko hata
ulegevu wa viungo vya mwili.
Kuna watu wengi ambao wana
ulemavu wa viungo vya mwili lakini kwa sababu ufahamu wao ni imara, hauna
ulemavu, wanaishi maisha ya furaha na ya mafanikio. Kwa upande mwingine kuna
mamilioni ya watanzania na walimwengu ambao wanaishi maisha yasiyo na msimamo
licha ya kwamba hawana ulemavu wowote, hii ni kwa sababu wana ulegevu wa
ufahamu.
Nguvu ya mawazo yako ni nishati muhimu sana katika kukuwezesha
kuyatimiza maono uliyonayo, yaani ili vitu na mipango uliyonayo ndani ya
ufahamu wako viwe halisi katika ulimwengu wa nje lazima uwe na ufahamu wenye
nguvu. Kuyabadilisha mawazo yako ili yawe kitu halisi lazima uwe na ufahamu
imara.
Ufahamu wenye nguvu ni
kani ya mabadiliko yoyote unayotaka
kuyapata katika maisha yako. Ukiwa mlegevu katika kuwaza na katika kuyawekea
msimamo yale unayoyawaza daima utakuwa mtu yule yule. Maisha yako yatakuwa juzi
kama jana na jana kama leo. Hautapiga hatua za mafanikio ya kiuchumi wala
kitabia kadhalika kimwonekano.
Ufahamu imara ni ule wenye mazoea ya kujipa muda kutafakari kwa kina
kila jambo unalotaka kulitekeleza. Kabla ya kufanya jambo ujizoeshe
kulitafakari kwa kina. Ufahamu kwa nini unalitenda, manufaa yake na athari
zake, changamoto zake pia ufahamu uhalali wa hilo jambo kiimani yako ya dini,
kitamaduni na kimazingira uliyopo.
Mtu mwenye ufahamu imara hatakiwi kufanya vitu kwa kukurupuka au kwa
kufuata hisia tu. Kwa bahati mbaya sana matokeo ya watu wengi kushindwa
kutimiza mambo waliojipangia ni kujiingiza kwenye hayo masuala kichwa kichwa
bila kuhoji na kujihoji. Mambo mengi sana yanayowaumiza watu leo ni matokeo ya
kufanya mambo bila tafakari ya kina.
Fikiri mtu anaanza mahusiano wa kimapenzi ghafla tu kwenye chombo cha
usafiri au kwenye mitandao au mtu anaanza mahusiano ya kimapenzi kutokana na
kuvutwa na kazi au cheo cha mwenzie, na wakati mwingine mtu anaingia kwenye
mahusiano kwa kuvutwa na mavazi maradadi ya mtu pekee.
Mipasuko mingi ya mioyo ya watu
kutokana na kuachwa, kuachana, kuachwa
au usaliti ni matokeo ya kutokufikiri vema kabla ya kuamua. Mimba nyingi
zinazotolewa leo ni matokeo ya kuingia kwichwa kichwa kwenye mapenzi na ngono
hivyo hata inapotokea mimba kuna kosekana utayari wa kulea.
Ufahamu imara ufanya maamuzi baada ya sala binafsi, utafiti binafsi na
kushauriwa na watu wenye hekima. Sehemu kubwa ya watu siku hizi hawalipi uzito
suala la sala na dua kabla ya kufanya maamuzi yaliyo mbele yao. Wengi hufikiri
sala haina cha kufanya na maamuzi wanayochukua jambo ambalo ni kosa kuu.
Ikiwa unaamini uliumbwa na
Mungu naye ni mkuu wa yote basi mshirikishe katika kila jambo. Sala ina nguvu
ya kuimarisha ufahamu kwa sababu inakufunulia vitu ambavyo huwezi kuviona kwa
macho ya kawaida, inakupa maonjo ya matumaini kadhalika inakuondolea woga.
Maisha ni mchezo wa tahadhari sana ambao hakuna anayeweza kushinda
bila kutumia uzoefu fikra angavu, elimu ,vipaji na na ushauri wa watu wengine.
Kutafuta ushauri kwa watu wenye hekima na uelewa juu ya jambo unalotaka kufanya
ni muhimu sana.
Kumbuka si kila mtu anaweza
kukushauri sahihi, si kila ndugu, mzazi, kiongozi au rafiki anaweza kukushauri
sahihi. Ili kujiimarisha kiufahamu jifunze kutaka ushauri kwa wenye hekima .
Kuhusu kutaka ushauri kwa watu pia ipo kasoro kwa baadhi ya watu, wao
hutaka ushauri juu ya jambo fulani kabla ya kujishauri. Wao ushauri wanaopewa
na watu wa nje wanauamini zaidi kuliko ushauri wanaojishauri. Ni muhimu
kujishauri wewe kabla ya kushauriwa, hata baada ya kushauriwa inakupasa
kupembua huo ushauri uliopewa, si kila unaloshauriwa ni sahihi.
Fahamu kuwa hakuna anayekufahamu wewe zaidi ya unavyojifahamu wewe
mwenyewe. Wewe unafahamu zaidi nini unapendelea na nini haupendi, moyo wako ni
mshauri wako wa kwanza ukiupa nafasi.
Usiruhusu watu wa nje watawale
maisha yako kwa kiasi kikubwa, maisha yako yanakuhusu zaidi wewe, usiamuliwe
kila kitu cha kufanya, namna ya kufanya na wakati wa kufanya. Uko tofauti.
Tafuta ushauri, sikiliza ushauri lakini kumbuka kuna wakati wa kufanya maamuzi
wewe pekee. Ukiwa msikiliza ushauri na mtekelezaji bila kujihoji mara
mbilimbili maisha yako hayatakuwa na msimamo.
Yako mambo mengine katika maisha yako yanahitaji maamuzi ya haraka na
magumu. Haya hauhitaji kutafuta ushauri. Masuala mengine unayotaka kufanya watu
hawawezi kukuelewa hata ukitumia miezi saba kufafanua ili wa kuelewe
hawatakuelewa, haya yanahitaji hekima yako kuyafanya.
Sio kila utakachotaka kukifanya katika maisha yako watu wa karibu yako
watakuelewa, yako ambayo hayaeleweki mwanzoni lakini yanaeleweka mwishoni baada
ya kwisha kutendeka. Hivyo usichelewe kufanya maamuzi kwa sababu unasubiri watu
wote wakuelewe na wakupe kibali.
Masuala ambayo ndani yako unayapa uzito sana lakini wengine wanaona ni
ya kawaida, ukingojea siku wakuelewe utabaki kama ulivyo siku sote. Unatakiwa
kujizoesha kuiamini akili yako, kichwa chako kina nywele na ubongo pia.
Chemchemi3.blogspot.com/
#Darasa la Maisha
Post a Comment