Unampenda au haumpendi, Dolnad Trump tayari ni Rais wa arobaini na tano wa Taifa kubwa la Marekani. Watu wengi hawaamini na bado hawakubaliani na kilichotokea, wengine bado wanaamini huenda Trump ataondolewa madarakani, yote hayo ni mawazo tu na ni kumpoteza muda kuendelea kuyafikiria. Ni ndoto za mchana.
Kutompenda kwako na kutomkubali kwako hakukuzuia nia yake ya kuwa Rais, hakukuzuia chama chake kumpitisha kuwa mgombea wala hakukuzuia kura zake za ushindi kadhalika hakukuzuia kuapishwa kwake hivyo pia hakutamzuia kafanya yale anayoamini ni sawa kwake.
Trump Enzi za utoto wake
Watu wadogo huzungumza kuhusu watu, watu wakati huzungumza kuhusu matukio na watu wakubwa huzungumza kuhusu hoja na ufumbuzi wa jambo jipya. Kumzungumzia sana Trump hakuna manufaa mapana hivyo napenda tuzungumzie mchakato wa Trump kuwa Rais na mafunzo ambayo unaweza kuyapata.
Bila kutazama watu wanasema nini kuhusu Trump mchakato uliomweka madarakani una mafunzo mengi na muhimu sana kwa maisha yako. Mafunzo hayo utayapata kama utakubali kujinyima hisia zako za kishabiki na kutafakari kwa kina kila hatua aliyopitia Trump kuwa Rais. Yafuatayo ni mengi kati ya hayo unayoweza kujifunza:
Umri wako usikuzuie kufanya jambo kubwa unaloliota. Afrika kuna watu wengi zaidi walinaogalagala kwenye hali ngumu ya kimaisha kwa kisingizio kuwa umri umewatupa mkono kufanya chochote. Vijana wengi wamekuwa waoga wa kufanya maamuzi yatakayobadili maisha yao wakihofia umri, umri mdogo kwao ni kizuizi tosha cha kutimiza ndoto zao.
Wazee wetu nao wakishafika miaka 50 na kuendelea wanaanza kujiandaa kifkra kufikia ukomo wa maisha lakini pia ukomo wa kutimiza ndoto zao kimaisha. Wanaume na wanawake wengi wakikaribia kustafu wanaanza kuyakatia tamaa mafanikio, wanapoteza uoni wa matumaini juu ya kufanikisha mambo walioshindwa kufanikiwa kwenye ujana, wanaishi maisha ya kukingojea kifo pekee.
Dolnald Trump ametoa somo zuri kwako, usiache kuota ndoto kubwa na kuzipigania kwa kigezo cha umri kuwa mdogo sana au kuwa mkubwa sana. Trump alikuwa mgombea mwenye umri mkubwa zaidi ya wote, ana miaka 70, wakati mpinzani wake Bi Clinton alikuwa na miaka 68. Unawezajifunza kitu hapo kwamba hauhitaji kuhofia kuchukua hatua fulani kwa kigezo cha umri. Chukua hatua.
Historia yako si hatima yako, uthubutu wako ndiyo hatima yako. Ukitafakari sana kwa nini watu wengi hawakumpa Trump nafasi ya kushinda kiti cha Urais, ni kwa sababu ya historia yake kisiasa. Ni mtu ambaye hajawahi kujihusiasha na siasa, hajawahikuwa mjumbe wa chama kwa ngazi yoyote, hajawahi kuwa seneta, wala gavana kadhalika Trump hatoki katika familia ya kisiasa kama Clinton au akina George Bush.
Unahitaji kufanya mambo bila kuwa mtumwa wa historia yako ya nyuma, wala hupaswi kufungwa na historia ya familia yako. Usifungwe na historia ya kabila lako. Usifikirie kufanya vitu kwa kuangalia nani alifanya, nani alifanya akashindwa au nani hakufanya kabisa.
"Wewe ni matokeo ya mambo yaliyopita lakini si mfungwa wa mambo hayo" Unaweza ukawa na hali fulani ya kimaisha kwa sababu ya makosa yaliyofanywa nyuma, unaweza kuwa maskini au ukakosa elimu kwa uzembe wa wazazi wako lakini usichoke kuota ndoto kubwa kwa sababu ya kuangalia ulikotoka.
Fanya maamuzi magumu kwa kuangalia unakoenda. Usifanye kwa kuangalia unakotoka.Trump hakusumbua kuogopa kuwa Rais kwa sababu hajawahi kuwa na cheo chochote kiserikali wala kichama. Hakusumbuka kuogopa kugombea kwa kuhofia familia yake haina historia ya kisiasa. Yeye aliamua kuandika historia mpya, na wewe unaweza kuandika historia mpya. Thubutu kwa vitendo.
Amini unachokitaka na taka unachokitaka. Watu wengi wanashindwa kutimiza ndoto kwa sababu ya kutojiamini, kwa sababu ya kutokiamini wanachokisimamia, na kutotaka wanachokitaka kwa kumaanisha.
Trump alijiamini mwanzo wa mchakato mpaka mwisho, hakuwa mtu mwenye kutegemea kufarijiwa na watu. Alijifariji, alijitutumua hatua za awali mpaka za mwisho, hakuyumba kimsimamo, wala hakuonyesha dalili za kukata tamaa. Trump alibaki yule yule kila mawio na machweo.
Usijifanyishe wala kupindisha vitu unavyoviamini ili watu wakupende. Amini unachokiamini na kiishi, huo ndiyo utambulisho wako. Watu wengi wanashindwa kutimiza malengo kwa sababu ya undumila kuwili, hawasimamii hoja bali wanasimamia hisia za kubashiribashiri.
Vile unaamini kuhusu jambo fulani jiweke wazi na jisimamie. Mambo ambayo alikuwa anayasimamia Trump katika kampeni zake yalikuwa yanatia ukakasi kidogo lakini ndiyo hivyo aliamua kuamini hivyo na hakubadilika na ni hayo yamempa Urais.
Usifanye jambo ukataraji kuungwa mkono na watu wote. Katika familia yako kuna watu hawatakuunga mkono katika mambo yote utakayoamua kutekeleza au katika mfumo wa maisha utakaoamua kuufuata. Hivyo pia ofisi, shuleni na popote ulipo.
Trump alipingwa na watu wengi, alipingwa ndani ya chama, alipingwa nje ya chama, alipingwa ndani ya Marekani na nje ya Marekani. Marais wastaafu wengi walimpinga, watu maarufu wengi walimpinga lakini hiyo haikumnyima usingizi. Aliendelea mbele hatimaye baadhi ya waliompinga walijumuika naye kwenye tafrija ya kuapishwa kwake. Baadhi ya waliompinga walikuja kumuunga mkono baadae. Baadhi walimpinga mpaka mwisho lakini haikuzuia yeye kuwa Rais.
Jitambue na zidisha juhudi katika unachokitaka bila kujali watu wangapi wanakupinga, shukuru kama wapo wanaokuunga mkono. Usipo kata tamaa ipo siku watakuelewa. Hata wasipokuelewa daima, hawatazuia kutimia kwa ndoto zako. Usiache kufanya michakato ya kutimiza ndoto zako kwa kungojea watu wote wakuunge mkono. Inatosha kama unaelewa nini unafanya. Songa mbele mpaka kieleweke. Kura yako mwenyewe moja ya Ndiyo inatosha kuzishinda kura elfu za Hapana.
Jiweka katika nafasi ya Trump katika kusaka Urais kisha kabiliana na mambo ya msingi unayotaka kufanya. Chagua kuamini katika ushindi. Donald aliamini katika ushindi mwanzo mpaka hatua ya mwisho ya ushindi wake. Hata leo ukimuona anavyojielezea, anazungumza kama mshindi wakati wate. Amewahikunukuliwa akisema hajawahi kushindwa katika jambo lolote. Jiamini na Mwamini Mungu.
chemchemi3.blogspot.com/
0746492600





Post a Comment