“Kila dakika ina thamani sababu ikitumika hauwezi kuirudisha” Willie Jolley
Upo hivyo ulivyo na hapo ulipo
kadiri ya matumizi yako yaa muda. Na kesho utakuwa kadiri ya matumizi yako ya
muda huu ulionao leo. Muda hauamui hatima ya maisha ya mtu, muda hautimizi
ndoto za mtu bali matumizi yako ya muda
ndiyo yanaamua hatima ya maisha yako.
Vile unavyotumia muda vizuri kwa
kufikiria mambo ya msingi na kupanga mipango ya kimaisha unayotaka kuitimiza
ndivyo utakavyofanikiwa. Kadiri
unavyotumia muda wako katika kujibidiisha kumuomba Mungu ndivyo utakavyofanikiwa.
Kadiri unavyoepuka kufanya mambo yasiyo na tija kwa afya yako, na katika
maendeleo yako ndiyo utakavyofanikiwa.
Kama wewe ni mtu ambaye unatumia
muda mwingi kulaumu wazazi, ndugu, marafiki, na serikali kwamba ndiyo sababu ya
wewe kutofanikiwa katika hali mbalimbali za kimaisha, unakosea sana na
unaendelea unapoteza muda. Kabla ya kulaumu watu wengine jichunguze kwanza matumizi
yako ya muda kisha ujilaumu wewe mwenyewe.
Jilaumu kwa kutokuwaza vizuri kwa
wakati, jilaumu kwa kwa kutofanya maamuzi mazuri kwa wakati sahihi, jilaumu kwa
kutokutenda kwa wakati. Ulishindwa kucheza na muda vizuri. Kabla ya kumlaumu
mtu mwingine unayehisi amehusika katika kukukwamisha kufikia kilele cha ndoto
zako jikague matumizi yako ya muda.
Jilaumu kwa kwa kutumia muda mwingi kupiga
soga, kuongea na simu, jilaumu kwa kupoteza muda kwenye mahusiano ya kimapenzi
ambayo yamekushushia heshima, jifinye kwa kupoteza muda mwingi kitandani badala
ya kupambana na changamoto za maisha, jilaumu kwa kwa kupoteza muda kwenye
mitandao ya kijamii(facebook, twiter, bmm, whatsup na instagram) badala ya
kufanya mambo yatakayokunufaisha. Pia usipoteze muda kwa kujilaumu tu kwa makosa yaliyopita,fikiria jambo jipya.
Hakuna muda usio na jambo la
kufanya. Hivyo mtu akisema wiki nzima, siku saba za wiki hana cha kufanya
anajidanganya mwenyewe. Ni dalili tu ya uvuvu, kujionea huruma, kujibweteka na
kutojitambua na wakati mwingine kufikiri umeshafanikiwa vya kutosha.
Mvivu analala hata saa kumi na
sita kwa siku hivyo kujikuta ana saa nane tu za kazi. Wakati kiafya inashauriwa
saa nane zitumike kulala kumi na sita zitumike kwenye kazi. Usikae bure,
usiache kupumzika lakini usiache kutumia muda vizuri, ni nyenzo nzuri ya
mafanikio.
Ili ufanikiwe katika maisha,
lazima ufahamu wewe ni nani na nini unataka maishani mwako. Hivyo kuna muda wa
kujitambua, kuna muda wa kutafakari nini unataka, kuna muda wa kukiombea
unachokitaka, kuna muda wa maandalizi wa kile unachokitaka kadhalika kuna muda
wa kukiita unachokitaka kwa vitendo.
Mungu ni mwenye haki, ametoa saa
24 za siku kwa kila mtu, maskini ana saa 24, tajiri ana saa 24. Msomi na asiye
na elimu wote wana saa 24. Kinachotutofautisha ni vile tunatumia hizo saa 24 za
siku. Wanaozitumia vizuri wanatoka, wanaozitumia
vibaya wanakwama. Hata leo umepewa saa 24 mikononi mwako, unazitumiaje ndivyo
utakavyokuwa kesho.
Matumizi mazuri ya saa 24 za leo yatafanya upige hatua
kadhaa mbele kuelekea mafanikio yako unayoyataka, kesho utaanzia pale
ulipoishia leo kama leo utaitumia vizuri. Kesho itakulazimu upige hatua ya
kwanza katika kukipata unachokitaka kama leo hauta leo itapita bila kufanya
jambo la maana.
Rafiki mpendwa wangu, muda
haumsubiri yoyote, unasonga mbele, hausimami kwa ajili ya yoyote wala chachote,
haumjui yoyote, haumpendelei yeyote. Inuka, tupa shuka, zinduka…..fanya
ukikumbuka uko nyuma ya muda hivyo inakupasa kukimbizana nao. Ni wakati wako
sasa. Wakati wa ndoto zako. WAKATI NI SASA. MUDA WA KUFANYA CHOCHOTE
UNACHOFIKIRIA NI HUU.
CHEMCHEMI3 BLOG@DARASA LA
MAISHA#HOSPITALI YA MAISHA
Post a Comment