Banner Salamu za mwaka mpya; Kwenu wafia nchi | Darasa La Maisha - Maisha Mafanikio

0
Bila usalama utafanya kazi gani, utalima vipi, utafanya biashara wapi na utamuuzia nani, bila usalama utasoma wapi na utaajiriwa wapi! Bila vyombo vya usalama makini tungekuwa tunaporwa mali zetu mchana kweupe, watu wangebakwa kila wabakaji watakapojisikia, ungeweza kulala ndani na watu wakakuingilia na silaha hata mchana kisha wakachukua mali zako kama zao.

Nimetafakari kwa kina lakini sijapata maneno ya Kiswahili wala ya lugha ngeni ambayo naweza kutumia kufikisha hisia zangu za ndani katika kuwashukuru wafia nchi.

Najua wengi tuna mapenzi na nchi yetu na tunajishughulisha katika kujiendeleza na kuiendeleza nchi, lakini wapo wanaotufanya tujione tuko salama kuwa Tanzania. Wanafanya hivyo hata kwa gharama ya uhai wao.

Nimefikiri juu ya ukweli kwamba wakati wa usiku watanzania wengi tunajirejesha majumbani mwetu, tukiamini ni wakati wa kupumzika, hata shughuli nyingi za kujitafutia kipato zinakoma tukisema ni muda wa kwenda kupumzika, lakini kwa upande mwingine wapo watanzania wenzetu wenye damu na ngozi nyeusi kama sisi wao wana kazi ya kuhakikisha tuko salama bila kujali ni usiku wala mchana.

Wakati kiza kinaingia wengi tunapanda vitandani kupumzika, wapendwa wenzetu hao kwa moyo wa ujasiri wanaviacha vitanda vyao, wanavaa kombati, wanabeba silaha mgongoni, wanaagana na familia zao kwa machozi ya ndani kisha wanaingia maeneo yao ya lindo.

Kheri ya mwaka mpya na shukrani za pekee kwenu ambao wakati wengi wetu wakati wa sikukuu ndiyo wakati wa mapumziko kikazi, wakati wa kukaa na watoto,wenzi, ndugu jamaa na marafiki ili tusherekee kwa pamoja, nyie wakati wa sikukuu familia zenu, watoto wenu, wenzi wenu, wazazi wenu hawapati kabisa ukaribu wenu.

Wakati wa sikukuu ndiyo unakuwa wakati ambao mpo kazini kweli kweli ili kuhakikisha sisi tunasherekee salama na ndugu zetu. Wapendwa wenu wanawakosa zaidi kipindi cha sikukuu, hamlali ili sisi na familia zetu tusherekee salama salmini.

Asante kwenu ambao kazi kwenu hazina sikukuu, baadhi tunafanya kazi ambazo zinatoa nafasi ya kupumzika siku za sikukuu lakini kwenu hakuna nafasi hiyo, ni kazi usiku na mchana. Nawashukuru nikiwatakia kheri ya mwaka mpya.


Watu wote tuna amini benki ni mahala salama pa kuhifadhi fedha zetu, hakuna mtu anayeiwazia kwa mashaka fedha aliyoiweka benki. Kipi kinafanya fedha iliyo benki iwe salama zaidi, ni kwa sababu kuna uhakika wa usalama unaotolewa na vyombo vya ulinzi.

Mnalinda fedha zetu katika mabenki wakati mwingine mifuko yenu ikiwa mitupu. Ndiyo, wala si jambo la kuficha, japo mnalipwa mshahara lakini mishahara yenu si mamilioni, kiasi cha kusema huwa hamuishiwi fedha mfukoni, wala si kweli kwamba hakuna wakati ambao watoto wenu wanakosa ada na mahitaji muhimu kwa sababu ya ukata.

Asanteni kwa sababu mnalinda mali na amali zetu katika hali ya kuwa nacho, hali ya kupungukiwa na hali ya kukosa kabisa. Ni uzalendo wa pekee sana na wa kiwango cha juu , ni uadilifu na utiifu uliotukuka sana kulinda mamilioni na mabilioni ya fedha za watu huku ukiwa huna shilingi!

Hivi karibuni yamejitokeza matukio kadhaa ya watu kuvamia benki, kuvamia vituo vya polisi, na katika uvamizi huo wapo askari waliopoteza maisha wakiitetea nchi na mali za wananchi, hivi tuna maliza mwaka kuna wajane na wagane kadhalika yatima ambao ni matokeo ya mapambano hayo. Zimepumzike kwa amani roho za askari waliokufa katika mapambano dhidi ya uharifu.

Najua askari ni binadamu kama mimi wanatoka kwenye familia kama mimi, wanategemewa kama mimi au mtu mwingine yeyote, hivyo anavyopoteza maisha kuna wengi wanaoumia nyuma ukiondoa taifa kupoteza nguvu kazi. Kheri ya mwaka mpya na dua njema ziziendee familia zilizopoteza wapendwa wao waliokuwa wakitumikia vyombo vya usalama.

Nimekutana na watu wengi waliowahi kutumikia vyombo vya usalama, hivi sasa wana ulemavu wa kudumu, na wengine wapo vitandani wakiuguza majeraha, lakini ukiwasikiliza mioyo yao ingali ina uzalendo wa kushangaza, wangali wana kiu ya kuitumikia nchi! Kwao kupoteza viungo si jambo la kuondoa shauku ya kulinda nchi.

Kheri ya mwaka mpya na dua ya uponyaji iwaendee makamanda mliopata majeraha katika kulinda mipaka ya nchi na mali za nchi.Wapumzike kwa amani makamanda wazalendo waliopoteza maisha wakilinda amani nchini Kongo, Comoro, Lebanon,  Sudan n.k.

Tunaojinasibu kwa maneno kuwa tu wazalendo ni wengi lakini wazalendo wa kweli na mnaothibitika bayana ni nyie wana usalama. Kazi zetu wengi zinaruhusu kugoma, au kuandamana inapotokea maslahi yetu kikazi imepunjwa.

Tunagoma kufundisha, tunagoma kuingia wodini, tunagoma kuendesha magari ya abiria, tunagoma kuingia viwandani ,ofisini n.k kwa sababu  ya mapunjo ya mshahara, posho au unyanyasaji fulani lakini nyie hamna nafasi ya kugomea chochote na popote. Ni kutii amri.

Maana mgomo wenu una hatari kuliko,hebu fikiri siku askari wa majeshi yote wamegoma, wameingia barabarani kuandamana .Hali ya usalama wa mipaka ya nchi itakuwaje, usalama wa raia sisi na mali zetu utakuwaje, usalma barabarani utakuwaje, magerezani kutakuwaje.

Ni hali tete isiyotamani itokee kwa mtu yeyote mwenye akili timamu. Mbarikiwe nyie mliotanguliza maslahi ya nchi mbele, mkaweka maslahi zenu nyuma.

Najiuliza hapo nilipo japo sina familia, ukiniambia nifanye safari ya ghafla kwenda nchi kama Congo au Somalia ,nitajiuliza, na pengine kimoyo moyo nitaomba kikombe hicho kiniepuke, na naamini tupo wengi wenye mioyo myepesi hivyo, ambao hatuna ujasiri wakusogelea mipaka ya nchi inayonuka damu kama Sudan kusini au Kongo.

Nahakika wakati huu tuna watanzania wanaolitumikia jeshi la wa wananchi, ambao wapo nje ya mipaka ya Tanzania, wakipigania usalama wa binadamu wenzetu ambao nchi zao zimeingiwa na dosari ya vita.

Tunao wana ulinzi wa amani kule Kongo na maeneo mbalimbali ya dunia, niwatakie kheri ya mwaka mpya. Mfahamu tuko pamoja, tunawaombea na tunawapenda pia.Tunaamini mtarejea salama. Mtaziona familia na familia zitawaona tena.

Tafakari kama barabara zisingekuwa na wana usalama barabarani, madereva wakorofi na wasio na mafunzo wangeteketeza roho za watu kiasi gani kwa uendeshaji wa hovyo hovyo na usioogopa sheria ikiwa ikiwa licha ya uwepo wa askari barabarani ajali ni kila leo, vipi wasingekuwepo. Asanteni na kheri ya mwaka mpya kwenu wana usalama barabarani.

Ni wazi magerezani kuna wasio na hatia na wenye hatia. Wapo waliosingiziwa na waliofungwa kwa haki. Magerezani kuna watu walioingia watukutu lakini sasa ni watu wazuri, wamebadilika kadhalika kuna wasiobadilika ambao wangali na hali ya uhalifu.

Najiuliza bila wana magereza huku mtaani tungeheshimiana kweli, kama kusingekuwa na magereza ,kama watu wasingeogopa kifungo sheria ngapi zingevunjwa, mauaji kiasi gani yametokea, wizi ungefanyika kiasi gani! Kheri ya mwaka mpya kwa wana kikosi cha Magereza.

Fikiri kikosi cha zima moto wanavyojitoa mhanga kukabiliana na majanga ya moto, asubuhi,mchana na hata usiku.Kikosi cha uhamiaji kinavyokabiliana na wahamiaji haramu, wengine wakija kufanya biashara ya ngono.

Madawa ya kulevya ni janga kuu hivi sasa, vijana wengi wanateketea lakini hebu fikiri bila Usalama wa Taifa, bila polisi, bila kikosi cha kupambana na madawa ya kulevya hali ingekuwaje? Vijana wangeharibikiwa kiasi gani, tungekuwa na mateja kiasi gani?

Bila vyombo vya usalama makini hakuna usalama. Usalama ukikosekana hakuna amani ,hakuna maendeleo, huwezi fanya maendeleo mahala pasipo salama. Hivi nani leo anafikiria kwenda kufanya biashara Somalia au Syria!

Nchi zilizokosa vyombo makini vya usalama, wanaukomo wa masaa ya kazi, saa moja jioni wanajifungia ndani, kwa sababu ya vyombo makini vya usalama na uadilifu wao, Tanzania hatuna hali hiyo .Asanteni wana usalama.
Chemchemi3.blogspot.com#Darasa la Maisha



Post a Comment

 
Top