Banner KWAKO MAFANIKIO NI NINI? | Darasa La Maisha - Maisha Mafanikio

0
 

"Mafanikio hayapimwi kwa kiasi cha fedha unachomiliki pekee bali watu uliobadilisha maisha yao" Michelle Obama.

 

Mafanikio ni hali ya kufikia hatua ambayo mtu ameitamani kwa muda , ni kupata kitu ulichokionea shauku kwa muda, ni kuwa katika hali uliyoitamani. Kifupi mafanikio ni kupata kitu ulichokitaka, ni kuwa na hali uliyokuwa na shauku kuifikia kadhalika mafanikio ni hali ya mtu kuwa wewe uliyemtaka, kuwa kadiri ya vile unavyojiona ndani yako kwamba unastahili kuwa.

Maana ya mafanikio haipatikani kupitia hali ya uchumi pekee. Kwa hiyo kuwa na fedha nyingi ni sehemu tu ya mafanikio lakini si mafanikio kamili. Unaweza ukawa na fedha lakini bado ukajiona umepungukiwa na jambo au hali fulani ndani yako.
Kwa hiyo kuitazama maana ya mafanikio kwa mlengo wa kiuchumi pekee ni kudogosha maana ya mafanikio, ni kudhoofisha maana ya mafanikio na ni sawa na kuyatazama mafanikio kwa jicho moja huku lingine ukiwa umelifumba kwa kiganja chako cha mkono makusudi.

Mafanikio ni msamiati mpana ambao hauna maana moja na kila mtu anatakiwa kuwa na maana yake, yaani kila mtu awe na hali au kitu ambacho kwake ndiyo mafanikio, haipaswi kujiita msaka mafanikio huku ukiwa hauna maana yako ya mafanikio .Usitafute mafanikio kwa kutumia maana za mafanikio za watu wengine.
Maana binafsi ya mafanikio izingatie unataka nini katika maisha yako, unahitaji kufikia hali gani ya kimaisha, hiyo hali au kitu unachokitaka unakitaka kwa nini na kwa wakati gani. Mafanikio yoyote yanakuwa na maana kama yana sababu za msingi za kuyataka, kutafuta mafanikio pasipo sababu za msingi za kutaka hayo mafanikio hudhoofisha hamasa binafsi ya kutafuta mafanikio.
 
 
Swali la Kwa nini unataka mafanikio unayoyataka, linahitaji pia lijibiwe sambamba na swali la wakati gani unataka uwe mtu fulani au uwe na hali fulani. Mafanikio pia yanahusu sana muda, usiseme tu nataka kuwa na kitu fulani bila kujiwekea ukomo wa muda wa kuwa umesha kipata jambo hilo si tabia nzuri ya mwana mafanikio.

Ukiwa unahitaji kiasi fulani cha fedha kwa ajili ya kutekeleza nia fulani uliyonayo lazima ujiwekee ukomo wa kuwa na hizo fedha.Ukiwa na shauku ya kufikia kiwango fulani cha elimu jiwekee muda ambao kivyovyote vile utakuwa umeipata hiyo elimu.
Hivyo pia kama unataka kujenga au kuwa mwandishi, mfanyabiashara mkubwa au mwanasiasa lazima uwe na ukomo wa muda katika kuifikia hiyo ndoto yako. Mafanikio yaliyofikiwa nje ya muda kusudiwa wakati mwingine hupunguza ladha ya mafanikio. Hali yoyote unayotaka kuifikia iwekee muda wa ukomo.

Baada ya kufahamu na kuwa na maana binafsi ya mafanikio ,tambua kuwa mafanikio ni mchakato si jambo la siku moja, hali ya kulala na kuamka nayo. Mafanikio ya kweli na ya kudumu yanachukua muda kwa sababu kila siku una jambo la kufanya ambalo linakuongezea kwenye ndoto zako. Kila siku ina thamani na imebeba siri ya mafanikio yako lakini ni kadiri utakavyoitumia.
Kwa mtu mwenye nia ya mafanikio kila siku anapaswa kuwaza na kuwazua ili apate wazo jipya litakalo mtoa kimaisha ,kadhalika imempasa kuwaza na kuwazua ili kupata mwendelezo wa mawazo ya mafanikio aliyonayo.
Ukipata nini leo kwako unaweza kusema umefanikiwa?
 

Simu; 0746492600, dailethmbele@yahoo.com






 

Post a Comment

 
Top