Banner Sonona chanzo cha watu kujiua na uwendawazimu | Darasa La Maisha - Maisha Mafanikio

0
Matukio ya watu kujiua kwa kujinyonga, kunywa sumu, kunywa madawa zaidi ya kipimo, kujichoma kisu n.k si mageni katika jamii yetu. Watu wanajitoa uhai kwa sababu zinazojulikana na zisizojulikana mfano wa hizo zinazojulikana ni visa vya kimapenzi, na ugumu wa maisha.

Kuna wakati tunasikia mtu amejiua lakini ukidodosa chanzo cha kujiua, unaweza kuwaza mbona halikuwa hata tatizo la kumfanya mtu ajiue. Pengine ni tatizo ambalo mtu angeweza kupona angepata msaada wa ushauri, lakini ndiyo hivyo anakuwa amejiua.
 
Waswahili wanasema hakuna kijiji kisicho na mwendawazimu. Ni msemo tu wa kumaanisha hakuna jamii isiyo na watu wenye kasoro fulani. Kwa mujibu wa tafiti watu wengi hivi sasa wapo kwenye hatari ya kuugua magonjwa ya akili ambayo hatimaye upelekea ukichaa wa kudumu.
  
Tatizo la afya ya akili linaloitwa Sonona, ambayo ni hali ya juu ya masongo wa mawazo kinaweza kuwa chanzo moja wapo cha matukio ya watu kujiua au pengine kuua kadhalika chanzo cha watu wengi kupata uwendawazimu wa kudumu.
  
Dr.Shita samwel, katika gazeti la Mwananchi, aliwahi kuandika makala hii yenye kutoa uelewa fulani juu ya maradhi ya ufahamu ya Sonona. Soma kwa makini.Kinga ni bora kuliko tiba.
  
Yapo matatizo ya kiafya ambayo jamii imekuwa ikiyapuuza kuwa siyo changamoto kubwa. Mojawapo ni Sonona ingawa kwa lugha ya kitabibu hujulikana kama Depression.
 
Tatizo hili huathiri afya ya akili na mwili kwa ujumla. Takwimu zinaonyesha kuwa athari zake hujitokeza kwa asilimia 10 ya jamii fulani duniani. Mara nyingi, huwakumba zaidi watu wenye umri kati ya miaka 10 na 24.


Depression kama wengi walivyozoea ni tatizo linalosababisha kushuka kwa hisia au mihemko ya kimwili hivyo mhusika kutojihusisha na shuguli yoyote suala linalomuathiri kimawazo, kitabia na hisia za mwili na kutojiona sawa kama walivyo watu wengine wanaomzunguka.
  
Mtu mwenye Sonona hukosa furaha, huwa muoga na kukosa matumaini. Mara kadhaa huwa hana msaada, hukerwa bila sababu za msingi, hujiona mkosefu, mwenye kuaibisha na asiye mtulivu.
  
Mtu mwenye tatizo hili anaweza pia kukosa hamu ya kujishughulisha na chochote ikiwa ni pamoja na kufanyakazi ambayo awali alikuwa akiipenda na kuifurahia.
  
Vilevile anaweza kukosa hamu ya kula au kula kupita kiasi. Anakosa umakini wa mambo, anashindwa kukumbuka masuala binafsi kwa kina na pia na mara nyingine akawa na tabia za kujaribu kujiua.
 
Mambo mengine yanayoweza kumpata mtu huyu ni kukosa usingizi, kulala kulikopitiliza, mwili kuumwa na uchovu mkali. Wakati mwingine huweza kuwa na matatizo ya usagaji chakula au nguvu za mwili kupungua.

Kupata Sonona ni zaidi ya kuwa na huzuni, kwa maana nyingine ni kukosa raha kulikopitiliza. Tatizo hili linamtokea mtu akiwa amepata dalili hizi mfululizo kwa zaidi ya wiki mbili.
 
Sababu zinazochangia kutokea kwa tatizo hili ni zile za kimwili (kibailogia) na kisaikologia. Kimwili ni pamoja na mabadiliko katika ubongo, kemikali zinazosafirisha taarifa na homoni (lakini bado haijulikani kwa kina sababu zakibailogia/kimwili zinavyosababisha sonona kutokea).
 
Mazingira tunayoishi ndiyo huwa chanzo cha matatizo ya kisaikolojia ambayo huweza kuwa kufiwa au kumpoteza mtu wa karibu, kupoteza kazi, kufilisika, kupokea taarifa mbaya na kuwa katika mazingira magumu.
 
Endapo hatua za makusudi hazitachuliwa kwa haraka mhusika huwa kwenye hatari ya kujiua au kuchanganyikiwa kiasi cha kupata uwendawazimu wa kudumu.
 
Chemchemi3.blogspot.com #Darasa la Maisha

  +255746 492 600

Post a Comment

 
Top