Banner FURAHA YAKO. TIBA YAKO | Darasa La Maisha - Maisha Mafanikio

0



"Kuwa na furaha ni uamuzi wako"


Furaha ya kweli na ya ndani ni kitu muhimu kushinda yote. Binadamu aliye hai na mwenye akili timamu furaha ni hitaji lake la msingi sana. Moyo wa mtu uliyejaa furaha huimarisha afya, hufukuza magonjwa na huimarisha mifupa ya mwili kumfanya mtu awe na nguvu kifikra na kimwili.


Furaha ni tiba na kinga dhidi ya maradhi; Watu wengi wasio na furaha, wale ambao mioyo yao imetawaliwa na huzuni huandamwa na maradhi mara kwa mara. Ukosefu wa furaha humfanya mtu kuugua .


Watu wengi wanaenda hospitali wakijihisi wagonjwa lakini baada ya vipimo vya kitabibu hugundulika hawana ugonjwa wowote mwilini. Baadhi hushindwa kukubaliana na matokeo hayo kiasi cha kujiingiza kwenye imani za kishirikina,bila kufahamu ukosefu wa furaha ni chanzo cha masumbufu yote.


Kwa bahati mbaya sana ukosefu wa furaha hautibiwi hospitali wala kwa waganga watu watumia gharama nyingi kwenye jambo lililo ndani ya uwezo wao.Mama mmoja mjane alinisimulia, kwa miaka alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa ambao kila madakatari walivyojaribu hawakuweza kuubaini.


Kwa bahati nzuri alikutana na tabibu mmoja aliyemfumbua macho. Huyu tabibu alifanya mahujiano na yule mama kwa saa tatu ndipo akabaini huzuni ya kufiwa na mume bado iko moyoni mwa Yule mama na ndiyo inamletea shida.


Tabibu akamshauri Yule mama aonane na mtaalamu wa saikolojia, baada ya kuhudhuria kliniki kwa muda alikuwa mtu mpya kabisa, mwenye furaha, mwenye uso unaoangaza kwa wingi wa matumaini zaidi alikuwa mwenye afaya njema.


Ukosefu wa furaha anaathiri uwezo wa akili kutenda kazi, unasabisha msongo wa mawazo, unaathiri uwezo wa kutunza kumbukumbu, unaathiri mahusiano yako na watu wengine, ni vigumu sana kuwasiliana na mtu mwenye huzuni kila mara. Ukosefu wa furaha unasabisha mtu kujitenga, kujiona hana thamani, na hata wakati mwingine kujiua.


Maisha bila furaha hayana maana. Kwa kweli maisha yanakuwa na maana mtu anapokuwa na furaha. Jambo la msingi ni kufahamu kuwa una haki ya kufurahi, na kwamba furaha ni moja ya zawadi uliyopewa na MUNGU .Maisha hayawezi kuwa sawa kila siku lakini bado haki yako ya furaha ipo pale pale, katika yote usijifunike blanketi la huzuni kila siku.


Mambo yafuatayo yanaweza kukufungulia milango ya furaha katika kuishi kwako, fahamu kuwa una wajibu wa kuifukuza huzuni kila ukiamka:


Usiishi jana. Kuishi jana wakati leo ni siku nyingine ni miongoni mwa sababu zitakazo kukosesha furaha maishani mwako. Kuishi jana ni kung’ang’ania mambo yaliyopita. Katika maisha kuna kukutana na matukio mengi yenye kutia huzuni, kuna kufiwa na wazazi,walezi, mwenza au mtu yoyote muhimu kwako. Kuna wakati unaweza ukatendewa ubaya usioelezeka kwa maneno.


Jambo la msingi ni kwamba kama bado uko hai jitahidi kuyasahau yaliopita, usiyape nafasi kama yalitokea jana. Shughulika nay a leo usigandamane na mambo yaliopita wakati una mengi ya kufanya leo. Maisha hayarudi nyuma, yanasonga mbele hivyo usiishi kwa kurudi nyuma.


Usipambane kubadilisha mambo yasiyoweza kubadilika. Katika maisha kuna mambo au hali zikitokea, mtu awe yeyote hawezikubadilisha. Mathalani huwezi kumfufua mpendwa wako aliyetangulia mbele ya haki.


Hauwezi kubadilisha kilichotokea wakati uliopita bali unaweza kubadilisha litakalotokea wakati ujao. Huwezirudisha wakati nyuma kamwe kwa hiyo kama kuna makosa uliyafanya wakati uliyopita usisumbuke kutaka kuyarekebisha, jambo la msingi tumia makosa yale kutorejea makosa.


Jipongeze kwa kila jambo unalofanikisha hata kama la onekana ni dogo machoni pa watu wengine. Watu wengi wanaishi kwenye dimbwi la huzuni kwa sababu hawana muda wakujichunguza kiundani, hawana muda wakuyatathimini mafanikio waliyonayo.



Wengi wanaumia mioyo kwa vichache walivyokosa wakati mkononi wana vingi vya kujipongeza. Anza kuoana thamani kwa kila mafanikio unayofikia, jipongeze kwa kila mafanikio ,jipongeze hata kama watu hawakupongezi.


Usitake vingi kwa wakati mmoja. Mafanikio ni mchakato wa hatua moja moja.Ukitaka kufanikiwa huku ukiwa na furaha moyoni mwako. Usiwe mtu wa kutaka ndoto zako zote zitimie kwa siku moja. Kumbuka Mungu aliumba ulimwengu na Mbingu kwa siku sita.


Na waswahili wanasema Roma haikujengwa siku moja. Jiwekee vipaumbele, uweke katika moyo wako na katika maandishi yale mambo ambayo unataka kuyatekeleza. Anza na jambo muhimu zaidi kwa wakati huu kulingana na maono yako. Kuwa na mipango mingi uwezavyo lakini jiwekee muda wa kulitekeleza kila jambo.


Usishindane na watu bali shindana na mipango yako. Ukitaka kuishi kwa furaha, mafanikio ya watu wengine yasikusukume ukaanza kushindana nao. Kushindana na watu wengine ni ukosefu wa hekima, unaoweza kukutoa kwenye mstari wa mafanikio unayoyataka. Kila mtu anaishi ndoto zake.


Ukinunua kitu fulani si kwa sababu ulipanga bali kwa sababu mtu fulani anacho, basi wewe utakuwa miongoni mwa watu wasioishi ndoto zao na wasiojitambua. Ukiishi kwa kushindana utakosa raha kwa sababu utakuwa unakitaka kila walionacho wengine badala ya kukitaka unachokitaka wewe.


Kutokusamehe ni sawa na kujinyonga. Unaposhindwa kumsamehe aliyekukosea unajiziba pumzi .Kutokusamehe ni sawa na kujifungia chumba chenye moshi mwingi huku madirisha yamefungwa. Ninasema hivyo kwa sababu madhara ya kutokusamehe yanamuhusu zaidi yule asiyesamehe na si asiyesamehewa.


Hata mtu akikukosea kiasi gani, kama utaamua kutomsamehe na kumwekea kinyongo ,mwisho wa siku wewe ndiye utakayedhurika kiroho, kiakili na kimwili. Kinyongo cha kutokusamehe kinasabisha magonjwa ya moyo, vidonda vya tumbo, presha na ukosefu wa furaha kwa yule asiyesamehe.

 

Watu wengi wanafikiri kutomasamehe mtu ni kumkomoa kumbe ni kujikomoa. Kama unataka uwe na furaha samehe hata kwa machozi. Kutokusamehe si ishara ya ujasiri kama wengi wanavyofikiri, bali ni ishara ya udhaifu.


 Unapomsamehe aliyekukosea unaruhusu hewa mpya iingie akilini mwako. Watu hatuwezi kujizuia tusikasirike, lakini tunaweza kujizuia kuwa na kinyongo. Msamaha ni kutii amri ya Mungu lakini pia ni ishara ya kuyajali maisha yako.


Yako mengi ya kufanya uwe na furaha lakini jambo kuu ni kufahamu kuwa furaha ni uamuzi wako, furaha haiji yenyewe inakaribishwa lakini pia furaha inawaza kufukuzwa. Furahia vile unavyoishi.


Kuwa na mtazamo chanya kwa kila unachofanya, amini katika ushindi hata wakati unaelekea kushindwa. Fukuza kila hisia za huzuni ndani yako, usipoteze muda kufikiria mambo yaliyokuumiza, fikiri juu ya mazuri unayoyatarajia.


 CHEMCHEMI3 BLOGSPOT.COM#DARASA LA MAISHA

Post a Comment

 
Top