Banner JINSI YA KUONGEZA THAMANI YAKO | Darasa La Maisha - Maisha Mafanikio

2
 
"Mtu wa kwanza kutambua na kuamini kuwa wewe ni wa thamani kubwa anatakiwa kuwa wewe mwenyewe. Jione na jiamini kuwa u mtu wa thamani kubwa na mwenye vingi, usikubali watu wakuaminishe kuwa wewe ni mtu wa kawaida usiye na thamani yoyote"

Maisha ya binadamu mwenye ufahamu timamu, mwenye kufahamu kwa nini anaishi na mwenye nia ya kufanikiwa lazima yawe na mwelekeo wa ukuaji. Mafanikio ni hatua ya juu ya mabadiliko chanya na ukuaji wa mtu kiakili, kiubunifu, kimaarifa na hata kitabia. Mafanikio ni mtoto wa ukuaji chanya na ni hatua ya ukuaji. 

Mafanikio yanahitaji maandalizi ya kina, mafanikio si jambo la bahati sana ni hali inayotafutwa kwa nia kwa kufanya michakato mbalimbali na kufanya mabadiliko mbalimbali. Mabadiliko yanapotua kwenye mikono ya mtu ambaye hajajiandaa vizuri huwa hayadumu, yanatoweka kama upepo na kuacha majeraha kwa muhusika.

Msomaji wa Chemchemi3.blogspot.com , Maisha ya mafanikio si maisha ya kubahatisha, kuhisi hisi, kusema sema na kukurupuka bali ni maisha ya kufikiri, mikakati, ni maisha ya vitendo na ni maisha ya kuchuchumalia mafanikio. Maisha ya mafanikio ni maisha ya kutafuta kujiongezea thamani kila siku.
Jiamini na jithamini
 

Unapofikiri kuwa miongoni mwa watu walifanikiwa katika eneo fulani, kiuchumi, kijamii , kisanaa, kitaaluma au kisiaasa lazima uishi maisha ambayo kila siku unakua. Kukua kwa maana ya kuwa tofauti na hali ya kimaisha uliyokuwa nayo jana, usiwe mtu yule yule kila siku.

Kudumaa katika maisha ni ugonjwa unaowakabili watu wengi na unazuia watu wengi kuwa watu wa kubwa katika jamii. Kudumaa kimaisha ni kuwa mtu yule yule kila kunapokucha, kuwa mtu yule yule ni kufikiri vile vile kila siku, ni kutenda mambo kwa maarifa yale yale wakati wote, ni kuishi kwa tabia zako zile zile bila kujitathimini na kujifanyia mabadiliko, ni kuridhika na hatua ndogo ya kimaisha na kutojishughulisha kupiga hatua zaidi. Huo ndiyo udumavu…kuwa mtu yule yule, kifikra, kimaneno, kimatendo, kimwenendo na hata kiimani huku ukiota ndoto kwamba siku moja utafanikiwa.

Kwa hiyo ni kufikiri kama ulivyokuwa ukifikiri miaka iliyopita, na kutenda mambo yale yale kwa namna ile ile bila kujali babadiliko ya nyakati na hali. Kadhalika ni kuridhika na mafanikio uliyoyapata kiasi cha kutojishughulisha na kutafuta kufanya kitu tofauti ya ulichofanya.

Maisha yako yanatakiwa kubadilika kila siku, kila siku ufikiri tofauti na ulivyokuwa unafikiri jana, kila siku uwe na hali na hamasa zaidi ya jana. Kila siku uwe mtu mpya kwa kiwango fulani. Mambo yafutayo unatakiwa kuyafanya ili kujiongezea thamani na kukua;

Badili mwenendo wako. Maisha ni mchezo wa makosa. Hakuna anayeweza kuifikia hatua fulani ya maisha bila kukosea, kufanya makosa ni sehemu ya maisha. Jambo muhimu ni kuepuka kurudia makosa yenye kukugharimu. Ikiwa una mazoea uliyojijengea au tabia uliyozoea ambayo imekuletea hasara mara kadhaa fikiria kuachana nayo.

Kuna tabia nyingi ambazo zinaweza kukushusha thamani katika jamii au familia yako. Ukiwa una tabia au mazoea yoyote ambayo hayana faida bali yana hasara amua kujinasua nayo. Tathimini tu hasara ngapi mazoea hayo yamekuletea, fikiri jinsi yalivyokupotezea hadhi katika jamii yako, tafakari ambavyo yameathiri maendeleo yako binafsi kisha chukua hatua. Mabadiliko yoyote chanya kitabia na kimwenendo yatakuongezea thamani mbele ya macho ya watu pia yatakuongezea kujiamini.
Usingojee watu watambue thamani yako kabla ya wewe kuitambua.
 

Kujiongezea elimu katika eneo unalotaka. Inaweza kuwa elimu ya darasani au nje ya darasa. Elimu haina mwisho, kila siku tunajifunza mambo mapya lakini hatufikii ukomo wa kujifunza. Kutafuta maarifa mapya ni jambo muhimu sana kwa mtu anayeteka kufanikiwa. Kama unataka kufanya biashara jifunze zaidi kuhusu biashara hiyo.

Jifunze mambo mbali mbali kwa kujiendeleza kupitia mifumo rasmi kama vile kujiunga na vyuo, unaweza pia kupata maarifa mapya kupitia kuhudhuria makongamano mbalimbali. Njia nyingine ya kujiongezea maarifa ni kujisomea vitabu, majarida, kusikiliza na kutazama vipindi elimu kupitia redio na televisheni.
 

Waweza pia kuzungumza na watu waliofanikiwa katika eneo ambalo unataka kujihusisha nalo. Ukitaka kuwa mwanataaluma wa habari au uchumi au elimu lazima ujielekeze kujua mambo yanayohusu fani yako. Kila tendo utakalofanya ili kujipatia maarifa mapya litakuongezea thamani.

Kugundua na kuendeleza vipaji vyako. Na vitumike kadiri ya ndoto zako. Na kadiri ya uhitaji ya watu wengine.Kipaji ni uwezo wa kufanya kitu fulani vizuri zaidi yaw engine. Kila mtu Mungu amempa kipaji chake, kila mtu ana uwezo ambao wengine hawana.

Kugundua kipaji chako ni nusu ya kugundua sababu ya Mungu kukuumba. Kama hujagundua kipaji chako basi bado hujafahamu kwa nini uliumbwa. Hatu ya pili baada ya kugundua kipaji chako ni kukiendeleza. Kugundua kipaji kunahusu kujitafiti ndani ili kufahamu vitu gani unahisi unavipenda zaidi kufanya, vitu gani unaweza kujifunza mapema, mambo gani ukifanya watu wanafurahia zaidi.

Unaweza kugundua kipaji chako kwa kuzingatia mambo ambayo unatumia muda mwingi kuyafanya au kuyafuatilia. Kukiendeleza kipaji chako ni kufanya vitu vinavyoendana na vipaji vyako, na kuchukua muda kujifunza zaidi kuhusu kipaji chako. Kutumia vipaji vyako kutakuongezea thamani mbele ya jamii pia kitakufungulia milango ya mafanikio. Kipaji ni ufunguo wa mafanikio.

Mafanikio yako yaguse maisha yawengine na kuyaathiri. Mwanamuziki wa kimarekani Ricky Ross, amewahikusema "Kipimo cha mafanikio yako si tu kuangalia vitu vingapi unamiliki bali ni kuangalia watu wangapi wamenufaika na mafanikio yako".

Jifunze kufikiria kuhusu wengine kwa vichache ulivyobarikiwa navyo. Kuna watu wanahitaji masaada wako, hilo lazima ulikumbuke. Huwezi saidia wote lakini inatosha ukitumia ulichonachokuwasaidia hata watu wachache kadiri ya uwezo wako. Wengine hawahitaji fedha, wanahitaji neon la faraja na maarifa tu kutoka kwako usiwakimbie. Kusaidia watu wengine kuwa na furaha, kusaidia wengine kufikia kufanikiwa ni mafanikio makubwa yenye kudumu kuliko hata kumiliki mamilioni. Unawezaokoa maisha ya wengine.
 
 

Ishi kwa kuyatenda unayoyaamini. Vitendo vyako ndiyo jina lako na heshima yako.Usiwe kifuata upepo wala usiwe mtu wa ndimi mbilimbili, watu wakuzunguka au unaofanyanao kazi au biashara lazima wafahamu unasimamia nini. Nini unapenda na nini haupendi. Watu hawajali sana nini unajua na nini unasema bali nini utenda. Watu wengi wanaishi maisha bila kuyapa uzito na matokeo yake jamii pia haiwapi uzito. Thamani yako ipo kadiri unavyojichukulia na kadiri unavyojiweka.

Usipokuwa mtu wa kufikiri na kuchukua maamuzi kisha kuyasimamia hayo maamuzi thamani yako haitaongezeka.Kusimamia unachokiamini ni moja ya mazoea yanayojenga heshima. Usiwe mtu wa kufanyiwa maamuzi na watu wengine katika kila kitu. Una nafasi ya kufikiri na kusimamia unachokiamini.

Jifunze vitu vipya. Kila siku jifunze vitu vipya.Usiitumie siku yako kwa kupiga soga na kuchati kwenye mitandao katika mambo yasiyo na faida. Maisha yanataka ujioe muda wa kutafakari na kujifunza vitu vipya kila siku. Siku iliyoisha bila kuingiza jambo jipya kichwani ni siku isiyo na faida.

Jenga mahusiano na watu wapya. Daima jaribu kutengeneza mawasiliano na watu. Kuongeza mtandao wa watu unaofahamiana nao, ni kujiongezea mawanda ya kufanikiwa. Fahamiana na watu wengi uwezavyo na uwatumie kukusaidia kutimiza malengo yako. Wengine wafanye washauri wako kadiri ya uzoefu wao na elimu zao, wengine wafanye wateja wako. Kuwa na mtandao mpana wa watu ni kujiongezea thamani.

Ongeza bidii kwa bidii. Chochote kile unachokifanya kifanye kwa kumaanisha na kwa bidii. Mambo yanaweza kushindikana lakini wewe zidisha bidii mpaka yatokee. Watu wenye kufanya mambo kwa kumaanisha na kwa bidii huheshimika sana. Hakuna jamii ambayo ni kipenzi cha watu legelege na wavivu. Maisha ni kumaanisha na kujibidiisha. Mtu anayeukaza mkono wake katika kutenda mambo hatakawia kufanikiwa. Chochote kila unachofanya fanya kweli usitanie.

Maisha yasiwe yale yale kila siku. Kila siku yafanyie mabadiliko. Kutoka hali ya kuwa hatua ndogo yaende hatua kubwa. Kutoka katika hali ya maisha yasiyoeleweka, yawe na maana. Kama maisha yako hayakuwa na furaha tafuta na mna ya kurejesha furaha na amani yako kila siku. Furahia maisha kwa kujiongezea thamani.
 
 
CHEMCHEMI3.BLOGSPOT.COM#DARASA LA MAISHA

Post a Comment

  1. I like your service thanks guys you are very critical

    ReplyDelete
  2. I have loved your class

    ReplyDelete

 
Top