Mafanikio yanafuatwa, yanatafutwa, yanaendewa, hayaji yenyewe. Mafanikio hayana mwenyewe bali ni kwa kila anayeamini katika kufanikiwa kwa vitendo.
Watu wengi hizi sasa akili, na ufahamu wao wote wameuelekeza mwaka 2017. Wanaamini mwaka 2017 utatatua shida zao zote za kiuchumi, kijamii, kimwili, kiroho na hata kimahusiano. Hii ni imani na ni jambo jema kuwa na matumaini kuwa wakati fulani masumbufu yako yataisha.
Imani ina kuwa na nguvu ya kubadilisha maisha inapoambatanishwa na vitendo na maarifa. Kuamini tu kuwa mwaka 2017 utabadilisha maisha yako bila kutathimini kwa nini mwaka unaoisha haukubadilisha maisha yako ni udhaifu. Msomaji wa chemchemi3.blogspot.com usitumie ulichonacho vibaya kwa kutegemea mwaka 2017 utakuletea kingine.
Maisha yako yatabadilishwa na wewe mwenyewe na si mwaka. Kabla ya kuamini mwaka 2017 utakuwa mzuri lazima uyaandae hayo mazuri unayotaka uyapate. Mwaka peke yake hauna uwezo wa kuyabadilisha maisha yako wala hauna uwezo wa kuyaandaa.
Mwaka ni nyenzo tu ya kuitumia kutimiza ndoto. Kama ambavyo ndoano ni nyezo au zana muhimu katika kuvua samaki, lakini hakuna ndoano inayojipeleka yenyewe mtoni au ziwani na ikaanza kuvua samaki.
Kama ilivyo kwamba ndoano hutumiwa na mwanadamu katika kuvua ndivyo ilivyo mwaka watakaoutumia vizuri watapata wanachokitaka ndani ya 2017. Watakao usubiri mwaka uwaletee wanayoyataka watasubiri hata 2050 wasipate.
Tusitiane moyo, wala kufarijiana kwa uongo na kujifariji kwamba 2017 ni mwaka wetu wa kutoka kimafanikio, wala tusiache kufanya tunayoyafanya katika kujipatia kipato kwa kutegemea kitu kinachoitwa mwaka 2017 kitakuja kutusaidia kuboresha maisha yetu. Haipo na haijawahi kutokea mwaka ukamfanikisha mtu asiyeishughulisha akili, asiyeshughulisha mwili.
Mwaka huu ni kama mwaka unaopita tu, una miezi ile ile, na siku zake zina saa zile zile, wiki zake zina siku saba zile zile kwa hiyo hauna tofauti unayokuja nayo ila tofauti utaileta wewe.
Hata kama mwaka 2017 ukawa na fursa nyingi, ukawa na hali nzuri kiuchumi bado fedha itawaendea wale walio na mikakati mizuri ya kuitafuta, mambo yataenda vizuri kwa wanaochakarika si kila atakae uona mwaka 2017.
Mwaka 2017 hauna uwezo wa kukuletea fedha mfukoni mwako, hauna uwezo wa kukuletea mke wala mume, hauna uwezo wa kukujaza furaha, hauna uwezo wa kukuletea watoto mapacha, wala hauna uwezo wa kukufaulisha mitihani wala kukupa ajira. Ni mwaka kama mingine tu wala hautoi mtaji wa biasharaka dhalika haukuzi mtaji.Mwaka 2017 hauna hautabadilisha hata kasumba mbaya za mwenza wako kama hajaamua kubadilika.
Mwaka 2017, haugawi viwanja bure, wala haujengei watu nyumba hata haulipii mtu kodi ya nyumba, haulipii mtu ada, haununulii mtu gari wala pikipiki hata baiskeli, haugawi chakula cha msaada nguo za mitumba kila kitu utaendeleea kujitafutia.
Yote unayotaka utayatafuta mwenyewe, kwa gharama zako, kwa maarifa yako, kwa imani yako na kwa wakati wako. Kadhalika utapata kadiri utakavyojibidiisha kuyapata, wala usifanye bidii ndogo ukategemea mwaka utakuongezea mafanikio. Mwaka 2017 hauna uwezo wa kutoa nyongeza.
Fikiri na tayarisha unachotaka kufanya mwaka 2017,kisha anza kukifanyia kazi kwa kujitaabisha kadiri ya uwezo na maarifa yako. Tathimini madhaifu yako ya mwaka unayoisha ambayo unahisi yamekukwamisha usifikie mafanikio fulani, jikosoe na jieleze ukweli ulipokose kisha kusudia kufanya mabadiliko.
Huko ndiyo kujiandaa kufanikiwa ndani ya 2017, kabla ya kuilamu 2016 ilikuwa ngumu kwako, anza kujisahihisha mwenyewe. Kuna ugumu mwingine uliuchangia mwenyewe. Usipojirekebisha utakuwa hivyo hivyo mwaka 2017, na utakapoisha 2017 utabaki kutumaini mwaka 2018. Zinduka.
Mwaka 2017 hauna kitu unaleta, vyote unavyovitaka utavitafuta na kujiletea mwenyewe. Mambo ni yale yale kila kitu kitapatikana kwa imani, akili, jasho, nguvu na uvumilivu. 2017, fikiria uanachokitaka, taka unachokitaka, penda unachokitaka, ishi ndoto zako.
NAKUTAKIA KHERI YA MWAKA MPYA 2017, UKAWE NA MWAKA WA MAFANIKIO KADIRI UNAVYOUWAZIA NA KADIRI UTAKAVYOPIGANIA HAYO UNAYOYATAKA.
CHEMCHEMI3.BLOGSPOT.COM #DARASA LA MAISHA#DAILETH I.MBELE
dailethmbele@yahoo.com
+255746492600
Post a Comment