Banner Magonjwa ya akili ya ngono | Darasa La Maisha - Maisha Mafanikio

2
  
“Kwa kitaalamu, ugonjwa wa akili ya ngono wa kupenda kuacha mwili wazi  unaitwa ‘exhibitionism’ ambapo mtu huweza kuamua kuacha maziwa, mapaja au kwa wanaume kuvaa suruali inayoelekea kuanguka kutoka maungoni,” Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akili na mtaalamu wa waathirika wa dawa za kulevya, Augustine Godman 
Kwa ufupi
·        Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akili na mtaalamu wa waathirika wa dawa za kulevya, Augustine Godman anasema, magonjwa ya akili kwa ujumla wake yanaweza kuzidi 1,886 lakini yapo yale ya ngono ambayo pengine yana changamoto lukuki kwa mwanadamu hasa Watanzania wasiofahamu kuwa ni magonjwa ya akili.
                                                          Daktari bingwa wa magonjwa ya akili
Huenda tumewaona wengi wao kama mashujaa, vijana wa kisasa au hata dada zetu wanaokwenda na wakati, kumbe ni wagonjwa wa akili.
Unasikiliza taarifa ya habari jioni. Unasikia kuwa, mwanamume amembaka mtoto wa miezi mitatu. Unaihoji nafsi yako… ni jambo gani lililosababisha akafanya ukatili huo? Je, ni tamaa kali ya ngono?
Wengine hudhani ni kisasi au imani za kishirikina na kwamba wahusika wametumwa.
Huu ni upotoshaji, lakini ukweli ni kuwa hayo ni magonjwa ya akili ya ngono ambayo yanawakumba asilimia 35 au zaidi ya Watanzania wote.
Watanzania hawa wanaugua magonjwa haya kwa wakati mmoja na kusababisha madhara mbalimbali kijamii, kiuchumi na migogoro katika familia na katika uhusiano.
Watu wenye magonjwa haya, si lazima watembee wakiokota makopo, kuvua nguo au kuwa na nywele ambazo hazijachanwa.
Hawa ni watu wa kawaida ambao tunafanya nao kazi, wenye uwezo mkubwa katika taaluma au pengine ni wazazi au hata walezi.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akili na mtaalamu wa waathirika wa dawa za kulevya, Augustine Godman anasema, magonjwa ya akili kwa ujumla wake yanaweza kuzidi 1,886 lakini yapo yale ya ngono ambayo pengine yana changamoto lukuki kwa mwanadamu hasa Watanzania wasiofahamu kuwa ni magonjwa ya akili.
Dk Godman anafafanua kuwa magonjwa ya akili ya ngono  kuwa ni yale yanayohusisha athari , upungufu  au mparaganyiko au  vitu visivyo vya kawaida  katika tendo la ngono.
“Mtu anaweza kuwa na  matatizo ya kihisia au ya kisaikolojia au vya kitabia katika  suala la ngono na huweza kusababisha madhara au kutopata mafanikio,” anasema Dk Godman
Daktari huyu ambaye amewahi pia kufundisha Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili (Muhas), kitengo cha magonjwa ya akili anasema  watu wengi wana magonjwa ya akili ya ngono, lakini hawajui kama ni magonjwa  na wanaendelea kuishi hivyo hivyo wakidhani ndivyo walivyo na baadhi wakipata matatizo katika jamii, wengine kufungwa jela au kupigwa kutokana na tabia hizo.
Mara nyingi tumekuwa tukiona wanawake wanavaa mavazi ya nusu uchi, wakizianika  nje sehemu kubwa za miili yao.
Tabia hizo ambazo  pengine huweza kuigwa na wengine  ni miongoni mwa magonjwa ya akili ya ngono kwani watu wanaopenda kufanya hivyo hujisikia raha na amani watu baki au wageni wenye jinsi tofauti wanapoyaangalia maungo yao na kushtuka.
“Kwa kitaalamu, ugonjwa wa akili ya ngono wa kupenda kuacha mwili wazi  unaitwa ‘exhibitionism’ ambapo mtu huweza kuamua kuacha maziwa, mapaja au kwa wanaume kuvaa suruali inayoelekea kuanguka kutoka maungoni,” anasema
Anasema, watu aina hii hutosheka kimapenzi mara tu wanapoona wanaume au wanawake wengine wameyaona maungo yao.  Hata hivyo, anasisitiza kuwa hutosheka pale tu watu wageni wanapoyaona maungo yao.
Mhadhiri wa Sosiolojia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Thomas Ndaluka anasema, baadhi ya magonjwa haya yanasababishwa na historia ya mtu.
Anasema hata hivyo mparaganyiko kama ule wa kupenda kuacha maungo wazi, unaambukiza kwa maana ya kuwa, anayeanza kufanya hivyo ni mgonjwa wa akili na matokeo yake wengine wanaiga.
 
Ubakaji wa watoto wachanga
Wengi wamekuwa wakihusisha ugonjwa huu na imani za kishirikiana, lakini ukweli ni kuwa, wale wanaowabaka watoto wadogo au kuwalawiti wana matatizo ya akili ambayo kitaalamu yanaitwa pedophilia (paedophilia).
“Katika hali ya kawaida si rahisi mtu mzima akamtamani kimapenzi mtoto wa miezi mitatu,” anasema mtaalamu huyo.
Ugonjwa huu unatokea pale mtu anapokuwa na hali ya kupata raha ya ngono kwa watoto wadogo wenye umri wa chini ya miaka mitano.
“Watoto wa jinsi zote huweza kuathiriwa na tatizo hili. Mtu mwenye ugonjwa huu huweza kuamua kumuingilia mtoto au tu kuamua kumchezea via vyake vya uzazi,” anasema Dk Godman.
Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk Kitila Mkumbo anasema sababu kuu za maradhi hayo ya akili ni pamoja na mazingira ya mtu wakati wa balehe, aliambiwa nini kuhusu tendo la ndoa na makuzi yake kwa jumla.
“Kwa mfano  inategemea kijana anaambiwa nini wakati wa balehe au yeye mwenyewe anaelewa nini maana ya tendo hilo” anaeleza Dk Mkumbo.
Anatoa mfano kuwa, wapo baadhi ya wanaume wanaamini au kufananisha kila shimo na uke.
“Huu ni ugonjwa mkubwa sana. Ndiyo maana utasikia mtu kambaka mbuzi. Yeye anaamini kila shimo linaweza kutumika kama uke”, anasema
Anafafanua kuwa magonjwa mengi ya akili ya ngono hujitokeza wakati wa balehe  na hukua kadri mtu anavyokosa matibabu.
Yapo matukio kadhaa yaliyowahi kutokea hapa nchini yanayoeleza watu waliowabaka watoto wadogo.
Kwa mfano, Desemba 2012, Yakobo Raymond alifikishwa mahakamani huko wilayani Muheza, Mkoani Tanga kwa tuhuma za kumbaka mtoto wake wa  kambo mwenye umri wa miaka mitatu.
Pia, huko mkoani Arusha, mwezi Januari mwaka jana, David  Samweli mkazi wa Moivaro Wilaya ya Arumeru, aliwabaka watoto wawili wa kike wa jirani yake na mtoto wake  wa kumzaa kwa nyakati tofauti chumbani kwake.
Licha ya matukio  kama haya kuripotiwa zaidi kwa wanaume wenye tabia hii, Dk Godman anasema wapo wanawake ambao pia huwabaka watoto wadogo wa kiume.
“Mwanamke anaweza kumvua nguo mtoto mdogo na kuanza kumshikashika tu, hapo huwa amepata  raha yake. Lakini pia anaweza kuamua kumwacha mtoto akiwa uchi,” anasema
Mtu mwenye ugonjwa huu humrubuni mtoto kwa vitu vidogo vidogo ili ampende na kumweka karibu naye na wakati mwingine baada ya kumfanyia vitendo hivyo humtishia kuwa akisema, atamdhuru.
 Tafiti mbalimbali zinaeleza kuwa, wapo watu katika nchi zilizoendelea ambao huasili  watoto, kisha kuwatendea vitendo hivi vya upedofilia.
 
Kufanya mapenzi na maiti
Ni jambo ambalo huzungumzwa au kutajwatajwa, lakini kumbe lina ukweli ndani yake.
Wengine wamekuwa na hisia kuwa linahusiana na imani za kishirikina au utumiaji wa dawa za kulevya lakini kumbe ni miongoni mwa magonjwa ya akili.
Wapo watu ambao hujisikia raha ya ngono kwa kufanya mapenzi na maiti. Watu hawa kwa kitaalamu huitwa ‘necrophilia’.
“Kwa kawaida ugonjwa huu huwa hauripotiwi mara kwa mara kwa sababu ya hofu ya kukiri kuwa umefanya mapenzi na maiti pia wanaotenda matendo hayo” anasema Dk Godman. 
Dk Mkumbo anasema kuwa magonjwa haya ya akili yana tiba ambazo zaweza kuwa ni za kisaikolojia,  sosholojia na kwa dawa.
“Kisaikolojia tiba ya watu hawa ni kupewa unasihi wajue kuwa wao ni binadamu na waache tabia ambazo kwa kawaida hazifanywi na binadamu” anasema Dk Mkumbo.
Kuwabaka wanyama
Hili limeshawahi kuandikwa na vyombo kadhaa vya habari na kuwashangaza watu wengi duniani ikiwemo pia katika Tanzania.
Zipo ripoti kadhaa za watu kuwabaka wanyama hasa wale wafugwao kama kuku, mbuzi, farasi na ngombe.
 Kwa mfano, Kijana mmoja mkazi wa mkoa wa Tanga alifikishwa mahakamani kwa tuhuma ya kumbaka na kumwingilia kinyume cha maumbile mbuzi wa jirani yake.
Katika tukio jingine, Yusuph Bakari mkazi wa Kata ya Kigera, Manispaa ya Musoma Mkoani Mara alinajisi kuku jike na kumsababishia maumivu makali na kusababisha afikishwe kwa afisa mifugo kwa uchunguzi zaidi.
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Absalom Mwakyoma alithibitisha tukio hilo.
 Huu ni  miongoni mwa magonjwa ya akili ya ngono na kwa kitaalamu ugonjwa huu unaitwa zoophilia na ni kosa la jinai katika nchi nyingi ikiwemo Tanzania.
Ndani ya daladala
 Wanawake wengi wamekuwa wakilalamika kuwa wanapopanda katika magari ya abiria hasa nyakati za asubuhi au jioni pindi mabasi yanapokuwa yamejaa kupindukia, wapo wanaume ambao huwasogelea na kuwabana kwa kiasi kikubwa.
 “Basi kama umewahi kukutana na hali hiyo ujue umekutana na wanaume wenye ugonjwa wa akili uitwao ‘ufroteri’. Ugonjwa huu wa akili huwakumba zaidi wanaume ambao hupenda kujisugua via vyao vya uzazi kwa watu wasio na ridhaa.
“Mara nyingi hutokea katika maeneo ya umma, au yenye msongamano. kila wanapogundua kuwa wameonekana wakifanya tendo hilo, hisia zao huisha hapo hapo na huondoka,” anasema mtaalam huyo.
 Anasema, mara nyingi watu hawa si kuwa hawana wenza  bali wanapata hisia zaidi wanapojisugua katika maumbile ya mwanamke ambaye hafahamu nini kinaendelea.
Kipigo, majeraha
 Umeshawahi kupata tetesi za wanawake ambao kila mara huamka na majeraha makubwa usoni na mwilini?
Usishangae kusikia kuwa mwanamke  huyo ana mwenza mwenye matatizo ya akili ya ngono.
Upo ugonjwa wa akili ya ngono ambao unahusisha vitendo halisi vya kujeruhi au kusababisha maumivu au kutoa manyanyaso.
“Kinachompa raha ya tendo hilo ni kumpiga mwenza wake, kumtukana wakati wa tendo au kumjeruhi, kumng’ata na kumuona akilia kwa uchungu au akitoka damu,” anasema Dk Godman.
Mtaalamu huyo anasema hali hii inapozidi huweza kusababisha  mauaji au majeraha ya kudumu na watu wengi hudhani ni manyanyaso ya kijinsia ya kawaida.
 Dk Ndaluka anasema watu wengi wa kundi hili wamepata maradhi hayo kutokana na historia za maisha yao.
“Wengine waliwahi kubakwa, kuteswa au kufanyiwa vitendo kama hivi na hawakupata msaada wa kisaikolojia kuondoa ule uchungu. Hivyo wanaweza kuwa na matatizo haya kiufahamu” anasema
 Hapa Dk Ndaluka anasema hatua za kisheria zinahitaji kuchukuliwa ili kumlinda mwenza ambaye huathiriwa.
Kupiga chabo
Upo ushahidi kuwa baadhi ya vijana hudiriki kutoa fedha kwa walinzi au wahudumu wa nyumba za wageni ili wawape ruhusa ya kuangalia watu wanaofanya mapenzi   katika vyumba.
Lakini tofauti na wengi wanavyofikiri huu si ukosefu wa maadili tu, bali ni ugonjwa wa akili ya ngono ambao mtu hupenda kuwaangalia watu wanaofanya mapenzi, ambao ni wageni machoni pake (si ndugu wala jamaa)  na kukamilisha raha ya ngono. Kwa kitaalamu ugonjwa huu wa akili huitwa ‘voyerism’.
Kwa mfano,  Mhudumu wa Nyumba ya wageni ya Savannah iliyopo  Tabata, Ndosi Yakobo  anakiri na kusema kuwa vijana huomba kuja kuwachungulia wapenzi wanaoingia humo.
“Ieleweke kuwa watu wa aina hii hawana nia ya kufanya ngono na watu wanaowachungulia, na wanapogundulika tu kuwa wanafanya hivyo zile hisia huisha papo hapo,” anasema
Watalaamu wa magonjwa ya akili wanaeleza kuwa watu wa kundi hili wanaweza  pia kupenda kuwatazama watu wakivua nguo au watu waliokaa utupu.
Mapenzi kwa njia ya simu
Wapo watu ambao hupata hisia za ngono kwa kuzungumza lugha ya matusi inayohusisha viungo vya mwili au vitendo vya kingono.
Huu ni ugonjwa wa akili ambao baadhi ya watu wanao pasipo kujua kuwa ni ugonjwa.
 Baada ya teknolojia ya simu kuvumbuliwa,  ugonjwa huu umekithiri na sasa watu wenye tatizo hilo wanatumia simu kufanya mapenzi au kuzungumza lugha ya matusi, kisha kupata hamu ya mapenzi.
Kitaalamu, mapenzi kwa njia ya simu huitwa, ‘telephone scatologia’ na hivi sasa watu wanaweza kujiunga na huduma fulani ambayo huzungumza njia za kufanya ngono au jinsi ya kumfurahisha mwenza na kumbe kwa njia hiyo watu wanatimiza haja zao.
Ugonjwa mwingine unaoendana na huu ni ule wa kupata hisia za ngono kwa njia ya mitandao ya kijamii. Wanatumia  intaneti kuzungumza habari za ngono hadi wanatimiza haja zao.
“Huu ni ugonjwa unaoathiri zaidi na unawaathiri vijana. Mara nyingi wakianza hawawezi kuacha hadi watibiwe,” anasema Dk Godman.
Hata hivyo, Dk Godman anaeleza kuwa yapo magonjwa mengine ya akili ya ngono madogo madogo ambayo yanaathiri watu wengi kwa mfano wapo watu wana mwamko mkubwa mno wa tendo la ngono kiasi cha kushindwa kulala wasipofanya hivyo.
 Dk Ndaluka anasema ni wakati sasa watu kupata ushauri wa kisaikolojia na matibabu na wakubali kuwa haya ni magonjwa ya akili na siyo tabia.
Naye Dk Godman anasema kutokana na uelewa mdogo  wa magonjwa ya akili ya ngono watu wengi wamefungwa kwa sababu ya kuwajeruhi wenza wao nakuwabaka watoto wadogo.
Dk Mkumbo anashauri kuhusu ugonjwa wa akili wa kuwabaka watoto (paedophilia) na kusema kuwa watu kama hawa wanaweza kuwa hatari katika jamii hivyo wanahitaji matibabu.
 Anashauri kuwa wazazi wawalinde watoto na waache tabia ya kuacha mtoto apakatwe au kuogeshwa na kila mtu.
“Hawa mapedophilia ni wengi hapa nchini, bila kupewa matibabu na sheria kuchukuliwa watoto wengi wapo hatarini” anasema
 Anasema licha ya matibabu ya kisaikolojia pia wagonjwa hawa huweza kupewa dawa za kupunguza kiwango cha vichocheo
 

Post a Comment

  1. elimu hii ni ya muhimu sana ienezwe zaidi.

    ReplyDelete
  2. tatitizo la kuangalia picha za ngono kwenye mitandao au simu za mikononi ni la ugonjwa gani?

    ReplyDelete

 
Top