"Kusamehe hakufanyi waliokukosea wabadilike tabia, bali kunalinda moyo wako usiumizwe zaidi na tabia zao"
Kutokusamehe hakufuti kosa ulilotendewa. Maisha hayarudi nyuma. Yaliyotokea yametokea, mwisho wa siku maisha lazima yaendelee na furaha yako irejee upya.
Fikiria kwamba wewe umeshika kaa la moto mkononi mwako, ukingoja kumrushia kaa hilo mtu aliyekukosea kwa kukutendea kitendo kibaya sana au kwa kukusemea neno baya.
Kwa bahati mbaya umelishikilia kaa hilo kwa muda mrefu lakini uliyemkusudia umchome nalo hajatokea. Unaweza tambua kiasi ambachoutakuwa umeumia!
Hivyo ndivyo watu wanaokaa na kinyongo bila kusamehe, wakingoja kulipiza kisasi wanavyojiteketeza, wanavyojiumiza, wanavyojiharibu mwonekano wao mzuri na wanavyoharibu ndoto zao bila kujifahamu.
Baada ya kuchapisha makala inayoelezea matokeo ya utafiti uliofanywa huko Marekani ukieleza uwezekano wa watu wasiosamehe kupata ugonjwa wa Saratani ama kansa kama ilivyozoeleka, mtu mmoja alisoma ile makala kisha alinipigia simu, akiwa na maswali mengi sana aliyotaka tujadili.
Moja ya maswali yake alitaka kufahamu ukiondoa uwezekano wa kupata saratani ikiwa hatasamehe ni madhara gani hasa mengine anaweza kupata, pili alisema akimsamehe huyo aliyemkosea atafahamu vipi kwamba alimkosea sana?
Na lingine akasema ni nini hasa faida ya kumsamehe aliyekukosea? Kwa kweli tulijadili kwa kina na kwa muda mrefu sana. Hatimaye akaniuliza swali gumu zaidi "kaka unafikiri nahitaji kusamehe hata kama mume wangu amehusiana kimapenzi na mdogo wangu kwenye kitanda changu...mmh..na bado hatakikuomba msamaha...!" Swali lake la pili lili malizikia na kilio upande wa pili wa simu.
Sitaki na siwezi eleza yote tuliyozungumza lakini naomba kwa faida ya wengine nijibu baadhi ya maswali hapa kwa manufaa ya watu wengine.
Kwanza ieleweke kuwa hakuna kosa ambalo halitakiwi kusamehewa, makosa yote yanasamehewa na ndiyo maana hasa ya msamaha. Ila yako mambo yanahitaji hekima zaidi katika kuendelea na maisha baada ya kusamehe.
Naomba nijibu hili la kwa nini usamehe na pengine linamwelekeo wa kutaka kufahamu faida za kusamehe;
Msamaha ni kama airfresh huleta hewa mpya na nzuri ndani ya maisha yako. Hebu chukulia umefunga mlango na madirisha wa chumba chako, chumba chako hakina singibodi, jua linawaka sana hivyo kuna joto kali, jasho linakutoka.
Kama haitoshi upepo umevuma umeingiza vumbi jingi sana ndani mwako na baada ya muda unabaini kuna panya amefia ndani anatoa harufu mbaya. Na sasa inakulazimu kuishi umo ndani kwa saa 24 bila kutoka au kufungua mlango!
Kwa hakika itakuwa wakati mgumu usioupenda, usiotamani ujirudie na haitakuchukua muda utaomba utoke. Maisha katika chumba kama hicho ndiyo maisha ya kila siku ya watu wasiosamehe.
Mara chumba hicho kikifunguliwa madirisha na milango, na ule mzoga wapanya ukatolewa utajisikia huru na amani kuwepo katika chumba kile kile. Hivyo ndivyo ulivyo umuhimu wa kusamehe.
Unaposamehe unaruhusu hewa mpya iingie katika maisha yako, tena msamaha unaleta harufu nzuri ya kufukizia maisha yako kiasi utajikuta unafuraha wakati wote. Msamaha ufungua ufahamu na kuleta mawazo mapya.
Unaposhindwa kusamehe unazuia ubongo wako kufikiri mambo mapya. Unaweza ukawa ufahamu wako haufunguki kuwaza mambo mazuri lakini kumbe umejifunga mwenyewe kwa kutokusamehe. Samehe uwe huru.
Samehe ili ujiepushe na mapigano na mikwaruzano ya nafsi. Unapokuwa hujasamehe au una mgogoro na mtu basi mara nyingi kuna kuwa na vita ya kimawazo dhidi ya huyo hasimu wako. Unatumia muda mwingi kufikiri ubaya wa kitendo alichokutendea, unafikiri zaidi juu ya namna utakavyomkomesha. Haya yote ni mambo yenye hasara kwako. Maisha ni mafupi usipoteze muda wa kufanya vita za ndani na mtu. Tumia muda uliopewa kuishi kwa kujihakikishia amani na furaha.
Msamaha huleta heshima na huleta amani ya kizazi hata kizazi. Heshima kubwa anayopewa mzee Mandela duniani kote ni kwa sababu aliwasamehe waliomfunga na kumtesa jela. Leo kizazi cha watu weusi, machotara na weupe wanachukuliana kwa upendo kule Afrika ya Kusini kwa sababu ya hekima ya mzee Mandela. Msamaha wako utanufaisha na kustawisha hata vizazi vijavyo.
Msamaha ni tiba.Kitaalamu magonjwa kama vidonda vya tumbo, kiharusi, kisukari na hivi karibuni wataalmu wamesema Saratani yanahusishwa zaidi na kutokusamehe. Kutokusamehe kunaathiri utendaji kazi wa ubongo na moyo.
Viungo hivyo vikiathirika mwili mzima unakuwa dhaifu. Usiudhoofishe mwili wako na afya yako kwa kutokusamehe. Usiweke rehani afya yako kwa kutokusamehe.Tafiti nyingi zinaonyesha watu wanaosamehe mapema wanaishi maisha marefu,ya furaha na wana afya imara.
Usipomsamehe au kumuomba msamaha leo huenda ukajijutia milele. Tusamehe kwa sababu hatujui kesho. Fikiri kwamba yule mtu ambaye umemuwekea kinyongo kwa muda mrefu, leo unapata taarifa amefariki dunia. Ndiyo, amefariki dunia ukiwahujamsamehe na dunia inatambua kwamba amefariki wewe ukiwa hujamsamehe.Utalia, utafurahi, msiban utaenda au utafanyaje labda!
Msamaha ni tendo la hekima na la kikubwa. Mama Joyce Mayer amewahisema, "Msamaha ni tabia za watu wakubwa na kinyongo ni tabia za watu wadogo". Watu wakubwa hawana muda wakubebelea kinyongo, wanafikiria hoja za maisha zaidi kuliko kufikiria watu.
Ufahamu wao umejaa mambo ya msingi hauna nafasi ya kuhifadhi kinyongo.Kama hujasamehe hiyo nafasi uliyohifadhi kinyongo ungeweza kuhifadhia mipango mizuri ya kimaisha.
Kutokusamehe ni utumwa. Mara nyingi watu wanaokosea wanasahau mapema kuliko watu waliokosewa. Sasa unakuta mtu aliyekukosea ameshasahau kama alikukosea na pengine hajali kukosea kwake, lakini wewe unamkumbuka kila siku, unamuwakia hasira kila leo, ukimkumbuka alivyokutenda, unashindwa kula, unashindwa kufanya kazi, unashindwa kusoma, unashindwa kulala, unashindwa kila kitu.
Ukimuona au ukimsikia, moyo unakupasuka, ukimuona unabadilisha njia. Ukimuona unakunja sura hata unaharibu sura yako nzuri.Wakati wewe unashindwa hayo mwenzako anaendelea na maisha kama kawaida, analala usingizi mnono, anafanya mambo yake vizuri, anakula na kunywa vizuri.
Kwa hali kama hii mtu akikukosea ukashindwa kumsamehe, unakuwa mtumwa, unakuwa unatawaliwa na huyo mtu. Yaani unampa nafasi ya kuendelea kukuumiza zaidi ya alivyokuumiza. Unamfanya aingie kwenye maisha yako. Samehe na uendelee na maisha mapya.
Kusamehe kunaongeza dunia yako, kutokusamehe kunapunguza dunia yako. Ukisamehe unakuwa huru kwenda popote, kufanya lolote na kusema lolote, lakini usiposamehe unadogosha dunia yako, unapunguza mawanda ya maisha yako. Ukisamehe haraka maumivu yanahama kwako na kwenda upande wa pili, wema kwa aliyekutenda ni kama kumpalia kaa la moto.
Usiposamehe unafanya vitu kwa wasiwasi, unaogopa watu, unatembea ukihofia kukutana na aliyekukosea. Ni maisha ya karaha.Ongeza mipaka ya dunia yako kwa kusamehe. Fikiri umesafiri kwenda mkoa ambao kuna mtu usiyepatana naye, fikiri umepata kazi kwenye kampuni ambayo kuna mtu mnahasimiana.
Samehe kwa sababu hata wewe umekosea mengi. Una uhuru wa kuendelea na kinyongo badala ya kumsamehe yule aliyekukosea kama una uhakika hakuna siku ambayo uliwahikumkosea mtu kwa kujua au kutokujua. Usisamehe kama una uhakika kwamba hakuna siku utahitaji msamaha kwa mtu aliyekukosea.Usisamehe kama hujawahikumkosea Mungu na akakusamehe.
Msamaha huleta furaha ya kweli. Huleta mwonekano mpya na mzuri. Msamaha huimarisha mifupa.
CHEMCHEMI3.BLOGSPOT.COM#DARASA LA MAISHA
dailethmbele@yahoo.com
+255746492600
Post a Comment