Tahadhari ya matumizi ya mitandao ya kijamii
Unatumia mitandao ya kijamii au unatumiwa na mitandao ya kijamii? Kila kitu kikitumiwa kwa kuzidi kina madhara, kikitumiwa kwa kiasi chaweza leta manufaa. Mitandao ya kijamii ikitumia vizuri inakuwa chanzo cha maarifa, ikitumiwa vibaya inakuwa chanzo cha ujinga wako. Mitandao ikitumiwa vizuri inafungua milango ya mafanikio, ikitumiwa vibaya inafunga milango ya mafanikio. Ikitumiwa vibaya inaua, ikitumiwa vyema inahuisha uzima.
1.Tawala matumizi ya mitandao, isikutawale
Baadhi ya watu wakiamka kitu cha kwanza ni kuingia, facebook, whatsup, instagram, bbm na kadhalika, haiwezekani siku kupita bila kuingia katika akaunti za mitandao. Mitandao inawatawala wao, inatawala hisia zao mpaka tabia zao.
Kimsingi mtumiaji wa mitandao ndiyo anapaswa kuwa mtawala wa matumizi ya mitandao. Tumia mitandao kama unavyotaka na si kama inavyotaka au kama watu wanavyotaka. Tumia mitandao wakati unaotaka na si wakati inaotaka.
2.Usianike katika mitanadao kila unachofanya
Kwa ajili ya usalama na faragha binafsi, ni vyema kutoruhusu watu wakufahamu kila kitu kuhusu maisha yako kupitia mitandao. Hii ni sana kuhusu kubandika katika kurasa zako za mitandao ya kijamii kila unachofanya.
Mathalani kuwaarifu watu wasiomuhimu kufahamu ju ya safari, mali unazomiliki, changamoto za kiuchumi au kimahusiano zinazokukabili. Ni jambo lisilo leta afya nzuri kijamii pale watu wasiohusika sana na wewe wanavyofahamu karibia asilimia 90 ya maisha yako kupitia mitandao ya kijamii.
Kwa mfano si lazima sana kuutaarifu uma kupitia mitandao ya kijamii kwamba umeanza mahusiano mapya ya kimapenzi, umevunja mahusiano na aliyekuwa mpenzi wako, kuonyesha kila unachofanya au kupanga na mwenza wako.
Mathalani kuna faida gani ya kubandika kila picha za mitoko ya faragha na mwena wako. Kuna faida gani kujibishana kwenye mitandao na watu waliokukosea, kwa nini msifanye faragha. Usifanye vita ya maneno na mtu au kikundi cha watu kwenye mitandao.
3.Si lazima uwe mtumiaji wa kila mtandao
Kila mchwao kuna mitandao mipya ya kijamii inabuniwa na kuenea. Hayo ni maendeleo ya teknologia huwezi kuyazuia. Cha msingi kufahamu ni kwamba si lazima uwe mtumiaji wa kila mtandao unaozaliwa. Epuka kuwa mtumwa wa kila mtandao, huu ni ulimwengu wa kuchagua, chagua unachokitaka, na tumia kinachokunufaisha. http://chemchemi3.blogspot.com/
Usitumie mtandao kwa sababu ni mpya au kwa sababu tu kwamba marafiki zako wanatumia huo mtandao. Una uhuru wa kutumia au kutokutumia mtandao huu au ule. Kutotumia baaadhi ya mitandao si ushamba, wala kutumia mitandao yote si uelevu, wakati mwingine ni aina fulani ya ulimbukeni.
4.Muda wa kazi ni kazi
Mara kaadhaa nimeenda dukani lakini nikacheleweshwa kupata huduma eti kwa sababu tu muuzaji alinisubirisha kunihudumia ili atume ujumbe whatsup au facebook! Wakati mwingine unaenda sehemu dukani au ofisini muhudumiaji anakuhudumia bila hata kukutizama usoni, macho yote kwenye simu ya kiganzani, anachat.
Watu hawapo makini kabisa na na kazi, kwa kweli matumisi mabaya ya mitandao ya kijamii ni miongoni mwa sababu kubwa ya kushuka kwa ufanisi wa kazi. Hivyo ni chanzo cha umaskini pia. Nimewahi kumshuhudia mgonjwa anahitaji msaada, nesi ana malizia kuchati ndo amuhudumie mgonjwa. Imekuwa hivyo hata kwa baadhi ya walimu wanachat darasani. Jizuie. Wakati wa kazi ni kazi.
5.Usibandike picha za utupu
Ukurasa wako wa facebook, whatsup au twiter au instra usiwe ulingo wa kubandika chochote. Lazima udhibiti matumizi ya picha mbaya kwenye ukurasa wako. Jipambanue kabisa kwamba wewe upo kinyume na picha hizo kwa kutozibandika, na watu wakikutumia usizishabikie na ikibidi kemea na hata inapobidi jiondoe kwenye kwenye makundi mitandao yasiyo na maadili.
6. Epuka lugha ya matusi na kashifa
Sheria ya mawasiliano ya mitandao ya nchi hii inatamka wazi kuwa kuandika matusi kwenye mitandao ni kosa ambalo adhabu yake linaweza kuwa kifungo cha miaka au kulipa faini. Ukiondoa hivyo matumizi ya lugha za matusi yanashusha hadhi ya mtu hivyo kutumia matusi kunaweza kukutupa jela au kukakushushia hadhi.
7. Watoto walindwe. Watoto wana haki yao ya faragha kisheria. Hivyo hata kama ni mtoto wako basi jaribu kulinda faragha yake. Usimtumie kila mtu picha ya mtoto wako. Usieneze sana picha za mtoto wako kwenye mitandao, watu wanaweza kuzitumia vibaya wakati fulani halafu mtoto akipata akili atakulaumu.
8.Matumizi yako ya mitandao yatengee muda
Usiwe mtu ambaye ukiingia kwenye mtandao,hautoki mpaka kifurushi chako cha internet kiishe. Bila kujali upo kazini, bila kujali unalea na bila kujali una mwenzi. Watoto siku hizi wanakosa malezi bora kwa sababu wazazi wakitoka kwenye mihangaiko wanajikita kwenye mitandao.
Hata ndoa zingine zinapooza hata watu kuhitajiana kwa sababu hawana muda wakuzungumza, wakiketi sebuleni kila mtu na simu, ipad au laptop mkononi , hakuna kuongeleshana, vidole vinaongea. Matumizi ya namna hii ni hatari kwa familia.
9.Usipige picha za utupu
Kuna kasumba mbaya sana miongoni mwa wwatu, wao wamejizoelea kupiga picha za utupu wakiwa faragha na wenzi wao. Wengine hujipiga picha hizo na kuziweka kwenye simu zao au ipad zao, wengine hawaishii tu kupiga bali huwatumia wapenzi wao picha hizo za utupu ili kusisimua hisia za mapenzi.
Haya ni mazoea mabaya na hatari sana, yanaweza kukugharimu wakati wowote endapo itatokea mtu mwingine akaziona hizo picha na kuziamishia kwake au kama ulimtumia mtu aliyekuwa mpenzi wako siku mkiachana anaweza asijali utu wako akaziachia.
Mitandao ya kijamii ni nyenzo ya kuboresha maisha, ni darasa huru la kujifunzia mambo mbali mbali ya kijamii na kiuchumi ili kuboresha maisha yako. Watu wanaoitumia vizuri wananufaika na wanapiga hatua za kimaisha, wanaoitumia vibaya wanakwama. Tumia mitandao ya kijamii kadiri ya ndoto zako, itumie kadiri ya unachopanga kufanya.
Blogu; http://chemchemi3.blogspot.com/
Email; dailethmbele@yahoo.com
Simu; 0746 492 600
Post a Comment