"Unaongozwa na fikra zako. Upo kadiri ya unavyojiumba mawazoni mwako"
Mawazo yako ni mbegu ya kila mambo mazuri au mabaya unayotenda. Kila kitu kinaanzia kwenye mawazo yako. Kauli nzuri na za hekima unazotoa ni matokeo ya vile unavyofikiri, kadhalika ikiwa wewe ni mtu uliyezoelea matukano, uongo na kauli zingine chafu yote ni matokeo ya unavyowaza.
Mwonekano wako, mathalani kujiamini au kutojiamini kwako ni matokeo ya unavyojiwazia. Vile unavyojiwazia ndivyo ulivyo na ndivyo utakavyokuwa. "Tatizo si watu wanakuwazia nini au wanakuwaziaje ila wewe mwenyewe unajiwaziaje" T.D. Jakes. Mawazo mazuri au mabaya wanayokuwazia watu wengine hayana nafasi ya kutengeneza au kuharibu maisha yako. Hivyo usipate shida nafsini ukigundua kuna mtu anakuwazia vibaya.
Mawazo mazuri au kujiwazia vizuri huleta maisha mazuri na mafanikio katika maisha. Mawazo yako au niseme fikira zako zina uwezo wa ajabu sana wa kubadilisha maisha yako katika mwelekeo chanya au hasi. Kila mtu hapa duniani anaishi mawazo yake. Kila mtu yupo kadiri ya anavyowaza kichwani mwake. Kumbuka mawazo ni mbegu ya yote na usisahau mbegu bora uotesha mche bora, mbegu dhaifu hufanya mche dhaifu.
Mawazo ni sawa na ujauzito. Mawazo ni ujauzito kwa sababu kila kitu kinaanzia kwenye mawazo yako kabla hatujakiona katika uhalisia. Mafanikio yote yanaanzia kwenye mawazo na kutokufanikiwa kote kwa kiasi kikubwa kunaanzia kwenye mawazo. Mawazo yako ni chemchemi ya mabadiliko yote unayohitaji maishani mwako.
Msomaji wa chemchemi3.blogspot.com/ Unaweza ukawa kwa kipindi kirefu unapambana na tabia fulani unayoitenda japo hauipendi. Yaani kuna mazoea mabaya ambayo pengine unatamani uyaache lakini hauwezi. Ni kwambie hautabadili tabia kwa kuanzia nje. Tabia hubadilishwa kwa kuanzia ndani. Kwa kuanza kuikataa ndani na kuijengea mtazamo hasi katika ubongo wako. Kabla ya kujikatia tamaa katika lolote basi fanya kwanza mabadiliko ya kiufahamu kasha jaribu.
Unaweza ukahama mtaa, ukahama chumba, ukabadilisha chumba na samani za ndani lakini bado mabadiliko ya kimaisha unayoyataka hautayapata kamwe kama haujabadilisha fikra zako. Kufanya mabadiliko ya nje bila kufanya mabadiliko ya ndani, bila kufanya mabadiliko ya kifikra ni sawa na kujipaka mkorogo ili uwe mtu mweupe. Mkorogo hauondoi ukweli kwamba wewe ni mtu mweusi na ipo siku utarejea tu kwenye weusi wako. Mtu aliyejibadilisha nje kabla ya ndani atabaki kuwa mtu yule yule.
Unaweza ukahama ofisi moja kwenda nyingine, kama wewe ni mwanafunzi unaweza kuhama kutoka chuo kimoja kwenda kingine au shule moja kwenda nyingine lakini bado utakabiliwa na hali ile ile uliyoikimbia kama hujabadilisha kufikiri kwako.
Siku hizi tumeona watu wakivunja mahusiano na huyu na kuanzisha na mahusiano mapya kila leo, kwa madai wapenzi wanaowapata wana kasoro kadhaa, wako wanaovunja hata ndoa kwa malengo ya kupata mtu tofauti. Kwa bahati mbaya hawajitafuti kasoro zao na kujitahidi kuzivua, hawajichunguzi kasoro zao na kuzivua ila wanataka mtu asiye na kasoro, matokeo yake ni kubadili wenzi kila leo.
Unaweza kunywa pombe sana, kuvuta bangi, ukafanya ngono holela, ukiamini ndiyo njia ya kupata furaha lakini bado usipate furaha. Zaidi utajisahaulisha kwa muda na hatimaye huzuni itakujia kwa kasi zaidi. Furaha inaanzia ndani hivyo kukaribisha furaha ndani ndiyo kutaleta furaha. Ni mawazo yako ndiyo yataleta furaha ya kweli.
Kubadilisha mavazi, nywele, rangi za kucha, maeneo ya kutembelea hakuwezi kubadilisha maisha yako. Kubadilisha jina lako, dini, dhehebu, chama cha siasa pekee havitoshi kubadili maisha yako kama haujabadilisha mawazo yako. Hivyo vyote vina nguvu kama umebadili kufikiri kwako.
"Tupo kama tunavyoamini kwamba tupo" Cardozo, mtu mweusi aliyewahi kuwa jaji mahakama kuu ya Marekani. Ni kwamba ulivyo nje ni matokeo ya ulivyo ndani, ndani kuna umba mwonekano wa nje. Badilisha ndani nje kutabadilika. Kubadilisha maisha ni kubadilisha kwanza unavyowaza. Tunatofautiana kimafanikio ya kiuchumi, kimahusiano na hata tunatofautiana viwango vya furaha kwa sababu tunatofautiana katika kuwaza na kuyasimamia hayo tunayoyawaza.
Kumbuka jinsi unavyo ishi ni kielelezo cha jinsi unavyofikiri. Huwezi kubadilisha maisha yako ya sasa kwa kutumia fikra zile zile zilizokusababishia hali uliyo nayo sasa. Badilisha unavyofikiri utabadilisha hali ya maisha na kitabia uliyo nayo.Yote yanaanzia kwenye mawazo yako.
chemchemi3.blogspot.com/ Darasa la Maisha
Kazi nzuri kiongozi
ReplyDelete